Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),imevunja rekodi
tena baada ya kukusanya kiasi cha Sh. trilioni 1.4 kwa Desemba, mwaka jana.
Hii ni baada ya kukusanya mapato ya Sh. trilioni 1.3
Novemba, mwaka jana ambayo pia ilikuwa rekodi serikali ya awamu ya tano
ilipongia madarakani na kufanya mabadiliko kwenye uongozi wa TRA na kudhibiti
ukusanyaji mapato.
Ni jambo la kupongezwa kwani ni miaka mingi viongozi
walijenga dhana kuwa Tanzania ni maskini isiyoweza kujitegemea.
Matokeo yake wananchi wamekuwa wakiishi kwa mateso
makubwa kwa kuaminishwa kuwa nchi kama Tanzania ni maskini na ilipaswa
kutegemea misaada ya nchi za nje.
Na hiyo ndiyo ikawa staili ya viongozi wengi
kuhalalisha safari za kwenda nchi za kigeni kusaka misaada `eti’ kwa kuwa nchi
yetu ni maskini.
TRA imepata mafanikio haya baada ya serikali kubana
eneo moja tu la bandari katika kuhakikisha watu wanalipa kodi kihalali. Mamlaka
hiyo imevunja rekodi ya kukusanya mapato ya awamu ya nne, ambayo kiwango chake
cha juu kilikuwa kati ya Sh. bilioni 800 na bilioni 900.
Tunaupongeza uongozi wa TRA na serikali katika
kuhakikisha kuwa kiwango kikubwa cha mapato kinakusanywa.
Fedha hizo tayari zimeanza kutumika kupunguza makali
ya maisha kwa Watanzania mathalani, zile zilizokusanywa Novemba
zimeelekezwa kusaidia utekelezaji wa ahadi ya Rais Dk. John Magufuli, ya kutoa
elimu bure.
Katika kutekeleza mpango huo wa elimu bure, serikali
ilitenga Sh. bilioni 131 ambazo zitatumika katika shule mbalimbali. Mpango huo
wa kutoa elimu bure unahusisha kutoa vitabu na kugharimia chakula.
Tunaamini katika serikali na TRA wakiendeleza kasi
hii ya kukusanya mapato, kuna uwezekano kabisa wa kuifanya nchi yetu
kujitegemea. Waasisi wa taifa hili, Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius
Nyerere na hayati Abeid Karume, ndoto yao kubwa ilikuwa kuifanya nchi yetu
ijitegemee.
Ndiyo Mwalimu Nyerere aliweka mkazo katika kilimo na
ujenzi wa viwanda kwa kuamini vingechochea maendeleo na kuifanya nchi yetu
kutotegemea misaada kutoka nje.
Hayati Karume naye alitumia zao la karafuu
kuiendeleza Zanzibar na ndipo alipoanza mradi wa ujenzi wa nyumba kwa ajili ya
watu wake na miundombinu.
Bahati mbaya katika miaka ya karibuni, viongozi
wengi waliopewa dhamana ya kuongoza nchi yetu walijielekeza zaidi katika
kujineemesha. Kwa sasa, si jambo la ajabu kusikia viongozi wakitumia mabilioni
ya fedha kwa kisingizio cha kwenda kusaka fedha za misaada nchi za nje badala
ya kuandaa mikakati ya kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuondokana
na aibu ya kuomba omba misaada nchi za nje.
Mathalani, serikali ikianza kubana mapato
yanayokusanywa na halmashauri mbalimbali nchini ina maana mapato ya serikali
yatapanda maradufu.
Bado hatujazungumzia kampuni mbalimbali ya
uwekezaji, ambazo zimekuwa zikipewa misamaha ya kodi na mengine
yanayolalamikiwa kama ya masuala ya gesi na madini.
Kwa mafanikio haya ya muda mfupi ya Serikali ya
awamu ya tano, inadhihirisha kuwa umaskini wa Tanzania unachangiwa zaidi na mipango
mibovu.
Tunaamini serikali ya awamu ya tano ikiendelea na
kasi hii itafanikiwa katika kipindi kifupi kutimiza ndoto ya Mwalimu Nyerere ya
Tanzania kujitegemea na kuachana na kuomba omba misaada.
0 comments:
Post a Comment