Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA), limetangaza
matokeo ya kidato cha pili huku msichana, Lineth Christopher kutoka Shule ya
Sekondari ya St. Aloysius Girl’s ya mkoani Pwani, aking’ara kitaifa.
Matokeo hayo yalitangazwa jana jijini Dar es Salaam
na Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dk. Charles Msonde, ambaye alisema waliofanya
mtihani huo mwaka jana walikuwa ni wanafunzi 363,666 sawa na asilimia 91.66.
Alisema kati ya walioufanya mtihani huo, waliofaulu
ni wanafunzi 324,068 sawa na asilimia 89.12, ambapo wasichana ni 164,547 sawa
na asilimia 89.00 na wavulana ni 159.521 sawa na asilimia 89.24.
Dk. Msonde alisema wanafunzi 39,567 sawa na asilimia
10.88 walishindwa kupata alama za kuwawezesha kuendelea na masomo ya Kidato cha
tatu; hivyo watarudia darasa wakati wanafunzi 33,104 sawa na asilimia 8.34
hawakufanya mtihani huo kwa sababu za utoro na magonjwa.
Alisema idadi ya watahiniwa waliopata ufaulu mzuri
wa madaraja ya Distinction, Merit na Credit ni 155,667 sawa na asilimia 42.80
ambao kati yao wasichana ni 68,780 sawa na asilimia 37.20 na wavulana ni 86.887
sawa na asilimia 48.60.
Alisema katika ufaulu wa masomo, somo la hesabu
limeshika mkia kwa kupata ufaulu wa asilimia 15.21 wa jumla wakati somo la
Kiswahili limefanya vizuri kwa kuwa na ufaulu wa jasilimia 86.34.
Aliongeza kuwa ufaulu wa masomo ya siasa, historia,
geografia, kingereza, fizikia, baiolojia, hesabu na utunzaji wa hesabu ‘Book
Keeping’ umeshuka ukilinganishwa na mwaka 2014, hivyo aliomba juhudi za
makusudi zifanyike.
Alisema ufaulu wa wanafunzi katika masomo ya msingi
ya Kiswahili, Biashara, na Kemia umepanda ikilinganishwa mitihani iliyopita.
Aidha, alisema wanaamini kuwa masomo yanayotegemea
maabara yatafanya vizuri hapo baadaye kutokana na juhudi za serikali
zinazofanyika za kuboresha maabara hizo.
WATAHINIWA KUMI BORA KITAIFA
Aliwataja kuwa ni Lineth aliyeng’ara kitaifa
akifuatiwa na Jerry Panga (Marian Boys Pwani), Rhobi James Simba (Marian Girls)
zote za Pwani.
Wengine ni Colin Emmanuel (Feza Boys Dares Salaam),
Nickson Maro (Magnifcat Kilimanjaro), Diana Mwakibinga (Morning Star
Mwanza), Elisha Peter (Buswelu Mwanza), Gaudencia Lwitakubi (Alliance Girls
Mwanza), Fuad Thabit (Feza Boys Dar es Salaam) na Geraldina Kyanyaka (Canossa
Dar es Salaam).
WASICHANA 10 BORA KITAIFA
Aliwataja wasichana bora kuwa ni Lineth, Rhobi,
Diana, Gaudencia, Geraldina na Renata Chikola ambao wanatoka (St. Aloysius
Girls).
Wengine ni Happyness Mwailunga (Canossa), Monica
Tesha (St. Aloysius), Judith Amos (Precious Blood) na Amina Khalfan (Fedha
Girls).
WAVULANA 10 BORA KITAIFA
Dk. Msonde aliwataja kuwa ni Jerry, Colin, Nickson,
Elisha, Fuad, Mwinangwa Chibunde (Mwanza Alliance), Baraka Muhammed (Eagles
Pwani), Joshua Kafula (Libermann Boys), Emmanuel Magombi (Morning Star), Frank
Charles (Marist Boys).
SHULE 10 BORA
Katibu huyo alizitaja kuwa ni Mwanza Alliance,
Mwanza Girls, Alliance Rock Army, St. Francis Girls, Bethel Sabs Girls, Don
Bosco Seminary, Shamsiye Boys, Feza Boys, Feza girls na Canossa.
SHULE 10 ZA MWISHO
Alizitaja kuwa ni Michenjele (Mtwara), Furaha (Dar
es Salaam), Ndando (Tanga), Mlongwema (Tanga), Kwai (Tanga), Lionja (Lindi),
Mkoreha (Mtwara), Mlungui (Tanga) Makong’onda (Mtwara) na Kwaluguru (Tanga).
Dk. Msonde alisema baraza linawasihi Maofisa Elimu
wa Mikoa na Wilaya wadhibiti ubora wa elimu kwa kufuatilia ili kuhakikisha
ufundishji katika maeneo yaliyotakiwa kutiliwa mkazo unafanyika.
Pia aliwataka wazazi kutoa ushirikiano kwa walimu
ili kuhakikisha mazingira ya ufundishaji yanaboreshwa.
0 comments:
Post a Comment