Miili ya wanajeshi wa KDF waliouwawa nchini Somalia
imepelekwa nchini Kenya na kupokelewa kwa heshima za kijeshi huku ikiarifiwa
kwamba operesheni kubwa ya kuwakomboa wanajeshi walionusurika ikiendelea huko
Somalia
Waziri wa Ulinzi wa Kenya Raychelle Omamo alizipokea
maiti za wanajeshi hao zilipowasili kwenye uwanja wa ndege jijini Nairobi huku
pia kukifanyika utaratibu maalum wa kutoa heshima za kijeshi. Waziri Omamo
akizungumza kwa huzuni kubwa aliwaomba wakenya waendelee kuwa na subira wakati
shughuli za ukombozi wa wanajeshi zikiendelea pamoja na miili zaidi ya
wanajeshi waliouwawa ikiendelea kutafutwa na kusafirishwa nchini humo.
''Huu ni wakati wa majonzi kwa jeshi la kenya na kwa
taifa letu kwa ujumla.Kwa mara nyingine tungependa kusisitiza shukurani zetu
kwa wakenya wanaotuunga mkono kwa upendo wao katika kipindi hiki chote kigumu
kwa wanajeshi wetu na familia zao.Kama nilivyowaeleza awali shughuli ya
kuwatafuta na operesheni ya uokozi zinaendelea na tunatarajia kuwapokea
wanajeshi wetu zaidi kadri siku zinavyokwenda.''
Omamo hakutoa lakini idadi kamili ya wanajeshi
wakenya waliouwawa ingawa ameweka wazi kwamba wanategemea maiti zaidi za
wanajeshi waliowawa kusafirisha nchini kenya .Kambi ya jeshi la Umoja wa Afrika
kusinimagharibi mwa Somalia ilishambuliwa na wapiganaji wa Al Shabab mapema
ijumaa hili likiwa ni tukio la hivi karibuni kabisa la kikosi cha Umoja huo wa
Afrika kushambuliwa ndani ya Somalia.
Hadi sasa serikali ya Kenya imekataa kusema
wanajeshi wake wangapi wameuwawa,kujeruhiwa au waliotoweka lakini kundi hilo la
Ashabab siku ya Jumapili lilitoa taarifa likisema zaidi ya wanajeshi 100
wakenya waliuwawa na wengine wameshikiliwa mateka.
Katika taarifa aliyoitowa rais Kenyatta amesema
kundi hilo halitopata muda wa kupumua na kuahidi kwamba nchi yake italipiza
kisasi ingawa haijafahamika hadi wakati huu ikiwa jeshi la kenya lililoko
Somalia limeifikia kambi hiyo inayoshikiliwa na wanamgambo.
Kadhalika kundi la Al Shabab limetoa kanda mbili za
sauti zilizorekodiwa likidai wanajeshi kadhaa wanashikiliwa mateka huku tovuti
zao ndani ya Somalia zikidai wanajeshi 12 wanashikiliwa mateka.
Waziri mkuu wa Somalia Omar Abdirashid
Sharmake amelaani shambulizi la Alshabab akisema ni kitendo cha kinyama huku
pia akitowa rambi rambi zake kwa familia za wanajeshi waliouwawa.Umoja wa Ulaya
ambao ni mfadhili mkubwa a jeshi la AMISOM umelaani shambulizi hilo ukisema ni
jaribio jingine la kuuhujumu mchakato wa kisiasa kuelekea somalia thabiti yenye
usalama.
0 comments:
Post a Comment