Nchini Burundi, hali ya sintofahamu imeendelea
kuripotiwa, hasa katika maeneo mbalimbali ya mji wa Bujumbura, kutokana na visa
mbalimbali vinavyoshuhudiwa ikiwa ni pamoja na mauaji, ubakazi na mateso
mengine wanayoyapata raia.
Watu watatu wameuawa na wengine wengi wamejeruhiwa
Jumatatu hii jioni katika mtaa wa 6 namba 89 tarafani Bwiza katika shambulio la
guruneti iliyorushwa na watu wasiojulikana.
Sehemu hiyo kulikotokea shambulio imekua ikilengwa
na mashambulizi mbalimbali hivi karibuni, na tayari watu kadhaa wamepoteza
maisha kutokana na mashambulizi hayo na wengine sasa wamepoteza baadhi ya
viongo vya mwili.
Katika shambulio la Jumatatu jioni, watu watatu,
ikiwa ni pamoja na afisa wa polisi wa cheo cha juu, afisa mwandamizi katika
wizara ya Elimu na mwanasheria mmoja wameuawa.
Msemaji wa polisi , pierre Nkurukiye, ameelezea
masikitiko yake kuona visa vya mauaji vimekithiri katika maeneo mbalimbali,
hususan katika baadhi ya maeneo ya mji wa Bujumbura.
Hata hivyo polisi imekua ikiendelea na operesheni
yake ya kamata kamata katika maeneo mbalimbali ya nchi. Lakini maeneo
yanayosakamwa sana na operesheni hiyo ni yale ambayo ni kitovu cha maandamano
dhidi ya muhula watatu wa Rais Nkurunziza. Vijana ndio hasa wanalengwa na
operesheni hiyo ya polisi. Mashahidi wanasema baadhi ya wanaokamatwa huukotwa
maiti siku chache baadaye.
Mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu yamekua
yakiinyooshea polisi kidolea cha lawama kuhusika na visa hivyo vya mauaji ya vijana
wanao kamatwa na baadaye kuokotwa maiti.
Wakazi wa mji wa Bujumbura wanasema wanatiwa hofu na
kukithiri kwa mauaji hayo ambayo wanaona kuwa yanaweza kusababisha kutokea kwa
mauaji ya kimbari au kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Hata hivyo mpaka sasa serikali bado imeendelea
kukataa kushiriki mazungumzo na muungano unaojumuisha wapinzani waliokimbilia
nje ya nchi (CNARED), muungano ambao serikali inasema unaundwa na watu
waliohusika katika jaribio la mapinduzi lililoshindwa Mei 13 na 14 mwaka 2015.
0 comments:
Post a Comment