Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John
Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Jeshi la Polisi hapa
Nchini IGP Ernest Mangu kufuatia kifo cha msaidizi wake Inspekta - Gerald Ryoba
aliyepoteza maisha katika ajali ya kusombwa na mafuriko ya maji wakati akikatiza
katika eneo la Kibaigwa,Wilaya ya Kongwa Mkoani Dodoma.
Katika ajali hiyo iliyotokea 03 Januari, 2016
Inspekta Ryoba akiwa na Mkewe na watoto wake wawili, pamoja na watu wengine
wawili walikuwa wakisafiri kutoka Geita kuja Jijini Dar es Salaam na walipofika
katika eneo la Bwawani gari walilokuwa wakisafiria kusombwa na maji na wote
sita kupoteza maisha.
Rais Magufuli amempa pole nyingi Mkuu wa Jeshi la
Polisi kwa msiba huo mkubwa, na amemuomba amfikishie salamu za pole kwa familia
ya Marehemu Ryoba na kueleza kwamba anaungana nayo katika kipindi hiki kigumu.
"Nimesikitishwa sana na tukio hili la
kuondokewa na msadizi wako pamoja na familia yake, ni tukio linalotia uchungu mkubwa"
amesema Mheshimiwa Rais.
Aidha, Rais Magufuli amemuomba Mwenyezi Mungu awape
nguvu na uvumilivu wafiwa wote, na aziweke roho za marehemu mahali pema peponi
Amina.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
06 Januari, 2016
0 comments:
Post a Comment