Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametembelea kiwanda cha
kusindika tumbaku cha mkoani Ruvuma na kuwasimamisha kazi
viongozi wa Chama Cha Kikuu Cha Ushirika cha SONAMCU.
Akizungumza katika ukumbi wa mikutano wa Ikulu Ndogo
ya Songea, wakati alipokutana na wakulima wa zao la tumbaku wa Wilaya ya
Namtumbo, Wananchama wa Vyama Vya Ushirika vya Mkoa wa Ruvuma, viongozi wa Mkoa
pamoja na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Edwin Ngonyani ambaye
ni Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini.
Waziri Mkuu amesema, Serikali ina dhamira ya kufufua
kiwanda cha kusindika tumbaku cha SONAMCU, na lengo la kutembelea kiwanda hicho
ni katika utekelezaji wa agizo la Rais John Pombe Magufuli la kufufua viwanda
nchini.
Waziri Mkuu Majaliwa, ametembelea maeneno mbalimbali
ya kiwanda hicho na kukagua mitambo iliyokua ikitumika kusindika tumbaku, kabla
kiwanda hicho kuzimwa miaka kadhaa iliyopita
baada ya kukosa malighafi za kuendelea na uzalishaji.
Pia,amemtaka Afisa Biashara kutoka Wizara ya Viwanda
na Biashara Bibi. Stela Lugongo kuandaa na kuwasilisha kwake mkakati wa kufufua
kiwanda hicho cha kusindika tumbaku, na baadae kuwasimamisha kazi viongozi wote
wa Chama Kikuu cha Ushirika cha SONAMCU waliohusika na tuhuma hizo na kutaka
wafikishwe Mahakamani.
“Serikali imeazimia kufufua viwanda, hasa vile
ambavyo havina wawekezaji vimebaki vyenyewe, Tunahitaji kujua namna ya
kuvifufua”. Alisema Waziri Mkuu huku akishangiliwa.
Waziri Mkuu Majaliwa pia, amesikiliza na kujibu kero mbalimbali za wakulima wa
tumbaku wa Mkoa huo, ambao walilalamikia
mfumo wa Vyama vya Ushirika na namna ambavyo vyama hivi vimekua
vikiwaibia fedha zao hadi kushindwa
kuendelea kulima zao la tumbaku na kukosa masoko ya mazao yao.
Aidha,Waziri Mkuu amewasihi wakulima kuwa watulivu
na kusubiri maamuzi ya Mahakama baada ya kuwa viongozi wa Chama cha Ushirika
SONAMCU ambao wamehusika na wizi wa fedha za wakulima kiashi cha Shilingi
milioni 800 kwa kipindi cha mwaka 2011 hadi 2014 tayariwamefikishwa Mahakamani
na uchunguzi unaendelea. Pia, amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Thabit
Mwambungu kukutana na wakulima hao ili kupatia ufumbuzi matatizo yao.
Aidha, ametoa wito kwa wakulima kuendelea kulima zao
la tumbaku kwa kuwa linaongeza pato la mtu mmoja mmoja, linasaidia kuchangia
pato la Mkoa na kukua kwa uchumi wa nchi. Amewashauri wakulima kuunda na
kuviendesha Vyama Vya Ushirika kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu
zilizopo.
Waziri Mkuu amemaliza ziara yake mkoani Ruvuma,
atafanya majumuisho ya ziara hiyo leo, kabla ya kuagana na viongozi wa Chama na
Serikali na kurejea jijini Dar es Salaam.
0 comments:
Post a Comment