Rais wa Sudan Kusin Salva Kiir ameteua wabunge 50
kutoka vuguvugu la waasi na kukubali kugawanya nyadhifa za uwaziri na wapinzani
wake kulingana na mkataba wa amani unaonuia kumaliza vita vya wenyewe kwa
wenyewe .
Kwenye tangazo kupitia radio ya serikali ya nchi
hiyo,Kiiir ametangaza uteuzi wa wabunge 50 waliopendekezwa na upande wa waasi.
Rais wa zamani wa Botswana Festus Mogae ambaye
anaongoza tume ya pamoja ya kufuatilia na kutathmini iliyoundwa na jumuiya ya
IGAD kuhakikisha mkataba huo unatekelezwa,amesema serikali itapewa nyadhifa 16
za uwaziri zikiwemo za ulinzi,usalama wa kitaifa,fedha na sheria huku waasi
wakipewa nyadhifa 10 zikiwemo za mafuta na maswala ya kibinadamu.
Wafungwa wa zamani kupokea nyadhifa
Kundi la wanasiasa wenye ushawishi mkubwa
lijulikanalo kama wafungwa wa zamani ambao walifungwa wakati mapigano
yalipoanza lakini wakaachiliwa baadaye,watapokea wadhifa wa maswala ya nchi za
kigeni na ule wa uchukuzi huku nyadhifa za maswala ya baraza la mawaziri na
kilimo zikiendea vyama vingine vya kisiasa.
Pande zote mbili za serikali na waasi kwenye mzozo
huo wa miaka miwili nchini Sudan Kusini zimelaumiwa kwa kuchochea mauaji ya
kikabila,kusajili na kuwauwa watoto na kutenda visa vya unajisi,mateso na
kuhamisha watu kwa nguvu ili kuwaondoa maeneo ya wapinzani wao.
Mzozo huo umesababisha mzozo wa kibinadamu huku watu
milioni 2.3 wakilazimika kuhama makwao na wengine milioni 4.6 wakihitaji msaada
wa chakula.Maelfu ya watu wameuawa na uchumi kuporomoka.
Pande zote zimelaumiana kuvunja mikataba
Kiir na kiongozi wa waasi Riek Machar wameshutumiana
kwa kuvunja mikataba ya amani lakini wanasema wangali wazingatia makubaliano ya
tarehe 26 mwezi Agosti,licha ya kushindwa kuafikia tarehe za mwisho
zilizowekwa.
Chini ya makubaliano hayo Machar anastahili kuchukua
wadhifa wa makamu wa Rais,wadhifa aliofutwa mwaka 2013.Kiongozi huyo wa waasi
hadi sasa hajasafiri hadi Juba kuchukua nafasi hiyo.
Hakuna muda uliyowekwa wa lini mawaziri watateuliwa
na kuchukuwa nyadhifa hizo.Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilianza mwei Disemba
2013 wakati Kiir alipomlaumu Machar kwa kupanga mapinduzi,hatua iliyosababisha
mauwaji ya kilipiza kisasi ambayo yameigawanya kikabila nchi hiyo masikini.
Serikali hiyo ya muungano,itadumu kwa muda wa miaka
3 kabla ya uchaguzi kufanyika na itakuwa na wizara 30.
Wachambuzi wamepongeza hatua hiyo lakini wakaonya
kuwa maswala mengi muhimu kwenye makubaliano ya amani hayajashughulikiwa.
Mwezi uliopita Kiir alifutilia mbali mfumo wa zamani
wa majimbo 10,na kuunda maeneo mapya 28 na hivyo kuenda kinyume na mkataba wa
kugawanya mamlaka.
Mapigano yanaendelea na mzozo huo sasa unahusisha
makundi kadhaa ya wapiganaji ambayo hayazingatii mikataba iliyoandikwa ya
amani,huku yakiongozwa na ajenda za maeneo yao na mashambulizi ya kulipiza
kisasi.
0 comments:
Post a Comment