Shirikisho la soka duniani Fifa litampta kiongozi
mpya leo wajumbe 207 watakapokusanyika mjini Zurich, Uswizi kumchagua mrithi wa
Sepp Blatter.
Blatter, 79, aliongoza shirikisho hilo tangu 1998.
Aling’atuka mwaka jana kutokana na tuhuma za ufisadi
zilizogubika shirikisho hilo.
Kuna wagombea watano wanaotaka kumrithi.
Watano hao ni Sheikh Salman bin Ebrahim al-Khalifa,
Gianni Infantino, Mwana mfalme Ali bin al-Hussein, Tokyo Sexwale na Jerome
Champagne.
Sheikh Salman na Gianni Infantino ndio wanaopigiwa
upatu kushinda.
Upigaji kura utaanza saa 12:00 GMT (saa tisa alasiri
saa za Afrika Mashariki).
Kabla ya kura kupigwa, kila mgombea atakuwa na
dakika 15 za kuhutubia wajumbe.
Kuna mataifa 209 wanachama wa FIFA lakini Kuwait na
Indonesia kwa sasa hawashirikishwi, hivyo wajumbe watakaopiga kura ni 207.
Ili kutangazwa mshindi duru ya kwanza, mgombea
anahitaji kupata theluthi mbili ya kura zilizopigwa.
Hili lisipofanyika, wagombea wote wanapigiwa kura
tena duru ya pili na anayepata kura nyingi kutangazwa mshindi.
Mshindi akikosekana duru ya pili, basi duru ya tatu
hufanyika bila mgombea mwenye kura chache zaidi raundi ya pili.
Fifa imesema lazima mshindi ajulikane leo Ijumaa.
0 comments:
Post a Comment