Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Afya Duniani WHO Natela
Menabde amesema, mpaka sasa, nchi 34 zimeripoti kesi za virusi vya Zika,
hususan bara la Amerika na Caribbean.
Katika taarifa yake kwa Baraza la Uchumi na Jamii la Umoja
wa Mataifa mjini New York, Menabde amesema Brazil imeripoti kesi zaidi ya elfu
4 za watoto waliozaliwa na vichwa vidogo, na mpaka sasa uchunguzi bado unaendelea
kuhakiki kama wana maambukizi ya virusi hivyo. Kabla ya mlipuko wa virusi vya
Zika, idadi ya watoto waliokuwa wakizaliwa na vichwa vidogo ilikuwa 163 kwa
mwaka.
Baada ya kutokea kwa mlipuko wa Zika, WHO ilianza kutekeleza
mkakati wa kimataifa kutoa mwongozo wa kukabiliana na kuenea kwa virusi hivyo,
na ulemavu wa viungo na neva zinazosababishwa na virusi hivyo.
Wakati huohuo, mwakilishi wa Umoja wa Ulaya nchini Brazil
Joao Gomes Cravinho amesema, Umoja huo utatoa dola za kimarekani milioni 10.7 kufadhili
utafiti kuhusu virusi vya Zika.
Cravinho amesema hayo baada ya kukutana na waziri wa afya wa
Brazil Marcelo Castro na mabalozi 24 wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya mjini
Rio de Jeneiro.
0 comments:
Post a Comment