Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa Staffan de Mistura
anaendeleza jukumu lake tete mbele ya mahasimu wa Syria,akitaraji maendeleo
thabiti yatakapatikana kuhusiana na masuala ya kiutu ili kuimarisha juhudi za
upatanishi.
Kwanza ilikuwa zamu ya kuzungumza na ujumbe wa
serikali ijumaa iliyopita,na jana ikawa zamu ya kuzungumza na upande wa
upinzani:Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa Staffan de Mistura amefanikiwa
kukiuka kiunzi cha mwanzo kwa kuzileta pande mbili hasimu katika meza ya
mazungumzo mjini Geneva.Leo hii amepanga pia kuwapokea mbali mbali wawakilishi
wa pande hizo mbili hasimu.
Hata hivyo utaratibu unaolenga kuzishirikisha pande
hizo katika mazungumzo ili kufikia ufumbuzi wa kisiasa nchini Syria bado ni
tete.Baada ya kukutana na de Mistura kwa muda wa masaa mawili jana,wajumbe wa
upande wa upinzani wa Syria wanasema wamepokea "risala ya maana"
kutoka Umoja wa mataifa,hata hivyo wanashikilia madai yao ya kuchukuliwa
"hatua za kiutu."
Msemaji wa wawakilishi wa upande wa upinzani wa kile
kinachojulikana kama "Kamati kuu ya Majadiliano" inayoungwa mkono na
Saud Arabia,Salim el Muslat anasema:"Ni muhimu kwetu na inaonyesha kwamba
jumuia ya kimataifa pia inalizingatia hilo kwa makini, yaani kuwaondoshea
usumbufu wananchi wetu-hiyo ndiyo sababu tumekuja huku-tunalizungumzia hili
kabla ya kuanza aina yoyote ya mazungumzo."
Madai ya kiutu yazingatiwe.
de Mistura anaonyesha kuunga mkono hoja hizo.Anasema
hata kama haitakuwa rahisi kuzuwia mizinga isifyetuliwe,hata hivyo juhudi za
kutaka raia waachiliwe huru ,itakuwa hatua ya mwanzo itakayoonyesha kuna
kinachotendeka upande wa kiutu.Mwishoni mwa mazungumzo pamoja na wawakilishi wa
upande wa upinzani Steffan de Mistura alisema "Kamati kuu ya
Majadiliano" imetoa hoja muhimu,ilipotaka,sambamba na mazungumzo,wananchi
wa Syria wanastahili kusikia na kuona mabadiliko nyumbani."
Ikionyesha ishara ya nia njema,serikali ya Syria
imeridhia jana kuruhusu "kimsingi" misaada ipelekwe katika maeneo
matatu yanayozingirwa ikiwa ni pamoja na Madaya.
Mkutano wa wafadhili utaitishwa alkhamisi ijayo London.
Wakati huo huo mkutano wa wafadhili umepangwa
kuitishwa London alkhamisi ijayo kwa lengo la kukusanya fedha kuwasaidia watu
milioni 13 na nusu wanaotaabika nchini Sria pamoja pia na wakimbizi milioni nne
na laki mbili wa nchi hiyo.Huo utakuwa mkutano wanne wa aina yake.
Mwaka jana Umoja wa Mataifa na mashirika yake
walitoa wito wa kupatiwa dala bilioni 8.4 kwaajili ya Syria,lakini
kilichokusanywa ni dala bilioni tatu tu nukta tatu.Waziri mkuu wa Uingereza
David Cameron atawakaribisha viongozi zaidi ya 70 akiwemo kansela Angela Merkel
wa Ujerumani,,katibu mkuu wa Umoja wa mataifa ban ki-Moon , waziri wa mambo ya
nchi za nje wa China Wang Yi na waziri mkuu wa Libnan Tammam Salam.
0 comments:
Post a Comment