Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ametoa shutuma kali
dhidi ya raia wake kuhusu jinamizi la ufisadi akiwa kwenye ziara rasmi ng'ambo.
Akihutububia kundi la Wakenya wanaoishi nchini
Israel, Rais Kenyatta alisema ni jambo la kusikitisha kwamba taifa la Kenya
linasifika kwa mambo mabaya ikiwa pamoja na ufisadi uliokithiri, ukabila wa
hali ya juu na matusi yanayoendelezwa hasa na wanasiasa.
Rais Kenyatta yumo katika ziara rasmi nchini humo.
“Sisi kama Wakenya pia, Mungu ametupatia nchi ambayo
ni nzuri mara 20 kuliko hii tuko hapa (Israel). Lakini tukitembea ni kulia, ni
kuiba ...,” alisema.
“… tuko na ujuzi pia, ya kuiba, ya kutukanana, ya
kufanya mambo mengine maovu, ya kuleta ukabila.
Bw Kenyatta alisema licha ya Kenya kuwa taifa lenye
utajiri mkubwa, kasumba ya ufisadi miongoni mwa viongozi na raia imelemaza
ustawi wa taifa hilo.
Kukiri kwa Rais Kenyatta akiwa ziarani Israel kwamba
ufisadi umemea mizizi katika taifa lenye uchumi bora zaidi kanda ya Afrika
Mashariki, kunajiri huku jinamizi hilo likiendelea kugonga vichwa vya habari,
na kutawala mijadala kwenye mitandao ya kijamii nchini Kenya.
Kashfa ya mamilioni ya pesa kuporwa kutoka mfuko wa
huduma ya vijana wa taifa (NYS) na vigogo serikalini, ndiyo sakata ya ufisadi
ya hivi karibuni inayokumba utawala wa Rais Kenyatta.
Mwaka jana, Kenyatta aliwapiga kalamu mawaziri
watano na maafisa wengine wakuu serikalini kutokana na madai ya ulaji rushwa.
Majuzi Jaji Mkuu Dkt Willy Mutunga alizua mjadala
mkali mitandao ya kijamii baada yake kunukuliwa na gazeti la Uholanzi akisema
kwamba Kenya ni taifa la “wanyang’anyi”.
Dkt Mutunga alinukuliwa akisema kwamba wananchi
wanapigana vita na magenge ya watu sawa na ‘mafia’ ambayo yanaongozwa na
viongozi wa kisiasa na wafanyabiashara wafisadi.
0 comments:
Post a Comment