Mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi Tanzania
Jaji Damian Lubuva amesema Rais John Magufuli hafai kuingilia kwenye mzozo wa
uchaguzi unaoendelea visiwani Zanzibar.
Akizungumza alipokutana na Dkt Magufuli katika
ikulu, Dar es Salaam Jumatatu, Jaji Lubuva amesema tume za uchaguzi zinafaa
kuwa huru na hazifai kuingiliwa kimaamuzi na Rais wala kiongozi yeyote.
Amesema wanaosema Rais anapaswa kuingilia kati
masuala ya uchaguzi iwe Tanzania bara ama Zanzibar wanafanya makosa, kwani Rais
hana mamlaka hayo.
“Unaposikia kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano
aingilie hilo suala la uchaguzi wa Zanzibar, yeye kwa kweli hana mamlaka
kabisa. Pili ni kama kujikanganya, huku unasema tuwe na tume huru isiyoingiliwa
halafu huku unasema aingilie kati maamuzi ya tume,” amesema Jaji Lubuva, kwa
mujibu wa taarifa iliyotumwa kutoka ikulu na kaimu mkurugenzi ya mawasiliano ya
ikulu, Bw Gerson Msigwa.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar Jecha Salim
Jecha alitangaza kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi uliofanyika visiwani humo
tarehe 25 Oktoba mwaka uliopita akisema kulikuwa
na kasoro nyingi.
Wiki iliyopita, Bw Jecha, kupitia tararifa,
alitangaza kwamba uchaguzi utarudiwa Machi 20.
Chama cha Wananchi (CUF), ambacho kimekuwa
kikisisitiza kwamba mshindi wa uchaguzi wa mwaka jana anafaa kutangazwa, kimesema
hakitashiriki marudio hayo ya uchaguzi.
0 comments:
Post a Comment