Shehena ya bidhaa aina ya mafuta ya Taa na dawa za kulevya
kilo 98 zilizokuwa zikiingizwa nchini kwa njia za panya kutoka nchini Kenya
zimekamatwa katika mapori yanayounganisha mpaka wa nchi jirani, katika
operesheni maalum inayofanywa katika vijiji tofauti vilivyopo mpakani ikiwa ni
sehemu ya kukabiliana na mtandao wa kihalifu unaojihusiosha na uingizaji wa
dawa za kulevya, wahamiaji haramu na ukwepeji wa kodi kwa serikali.
Wakizungumza katika eneo la Horohoro mpakani mwa Kenya na
Tanzania timu ya watendaji wa mamlaka ya mapato nchini (TRA), maafisa uhamiaji
na wakaguzi wa mamlaka ya chakula na dawa nchini tawi la Horohoro, wamesema
lengo la operesheni hiyo ni kuhakikisha kuwa mipaka ya nchi inakuwa salama
kufuatia kubainika kuwepo kwa mtandao wa ukwepaji kodi, kupitisha wahamiaji
haramu na vikundi vya uhalifu.
Kuhusu kukamatwa kwa dawa za kulevya mratibu mwandamizi
msaidizi wa idara ya uhamiaji nchini tawi la Horohoro Mwesiga Lubalila amesema
katika zoezi la kukabiliana na uingizaji wa bidhaa haramu, kundi la watu
waliokuwa na pikipiki zilizokuwa zimebeba maboksi walipobaini mtego wa
kukamatwa walilazimika kuzitupa pikipiki hizo na kisha kukimbia ndipo walipopekua
na kukuta dawa za kulevya aina ya Mirungi kilo zenye uzito wa kilo 98 iliyokuwa
imefungwa katika vifurushi vyenye uzito wa kilo mojamoja kila kimoja.
Kufuatia hatua hiyo mkaguzi mkuu wa mamlaka ya chakula na
dawa Bwana Thomas Nkondola amesema bidhaa zote zinazoingizwa kutoka nchini
Kenya hazitaruhusiwa kuingia endapo kama hazijafanyiwa ukaguzi kufuatia baadhi
ya wafanyabiashara kuingiza bidhaa zilizopitwa muda wake na hivyo kuhatarisha
afya za watumiaji.
0 comments:
Post a Comment