Shirika la Msamaha Duniani limesisitiza kuwa, uvunjaji
mkubwa wa haki za binadamu unaotokea katika kona mbalimbali za dunia unafanyika
kwa msaada wa silaha za nchi za Magharibi na kwamba Magharibi ndiyo inayopaswa
kubeba dhima ya machafuko yote hayo.
Salil Shetty, Katibu Mkuu wa Shirika la Msamaha Duniani la
Amnesty International amesema hayo kwenye mkutano wa amani wa mjini Munich,
Ujerumani na kuongeza kuwa, nchi za Magharibi ni moja ya wabeba dhima wakuu wa
mapigano na machafuko yanayotokea katika kona mbalimbali za dunia.
Amesisitiza kuwa, sehemu kubwa ya vitendo vya uvunjaji wa
haki za binadamu vinavyotokea duniani leo vinafanywa kwa kutumia silaha ambazo
madola ya Magharibi yanawapa wanaotenda jinai hizo.
Ameongeza kuwa, jambo la kusikitisha zaidi ni kuona kuwa
baadhi ya magenge hayo yanayofanya jinai yamepewa mafunzo na majeshi ya nchi za
Magharibi.
Katibu Mkuu wa Shirika la Msamaha Duniani amesema kuwa,
dunia hivi sasa imekumbwa na mgogoro wa ukosefu wa usalama na wimbi la
wakimbizi na kwamba ni wajibu kwa jamii ya kimataifa kuwalinda raia na watu
wasio na ulinzi.
Amesema, zaidi ya asilimia 90 ya wakimbizi hukimbilia nchi
jirani na hawatii mguu wao katika nchi za Magharibi (licha ya nchi hizo za
Magharibi kuwa wachangiaji wakuu wa jinai zinazotendeka duniani leo).
0 comments:
Post a Comment