Na Mwandishi wetu Washington
Kila ifikapo tarehe 14 Februari nchini Marekani na sehemu
nyengine Duniani husherehekewa Siku Ya Wapendanao "Valentine's Day",
au kama ijulikanavyo kwa jina jengine "Siku Ya Mtakatifu Valentine"
(Saint Valentine's Day). Katika miaka ya hivi karibuni siku hii pia imeanza
kusherehekewa katika maeneo ya Afrika Mashariki. Labda shukrani ziende kwa enzi
za utandawazi. Lakini je Siku Kuu hii ilianzia lini?
Asili yake.
Hakuna chanzo cha uhakika kuhusu asili na chimbuko la Siku
ya Wapendanao.
Hata hivyo inaaminika kuwa asili yake inarejea katika enzi
za Himaya ya Warumi,na baadaye Kanisa Katoliki kuingiza katika Ukristo.
Kuna watu watatu katika historia ya Kanisa Katoliki ambao
wanajulikana kama Mtakatifu Valentine au Valentinus, na wote inasadikiwa
walikufa kama mashahidi kwa mujibu wa itikadi za Kikatoliki, na kwa hivyo Kanisa
likaamua kuiadhimisha siku waliyonyongwa kama kuwaenzi watumishi hao.
Kuna nganu inayodai kuwa Valentine alikuwa ni Mchungaji
aliyehudumu Roma katika karne ya tatu. Wakati huo, Mfalme Claudius Wa Tatu,
alipitisha amri ya kupiga marufuku ndoa kwa vijana wa Kiume kwa vile alihisi
kuwa wanaume wasio na wake au familia walikuwa askari bora zaidi kuliko
waliokuwa kwenye ndoa.
Mchungaji Valentine hakukubaliana na amri hiyo ya Mfalme na
akawa naendelea kufungisha watu ndoa kwa njia za siri. Mfalme Claudius alipogundua
mpango huo, aliamuru Valentine anyongwe.
Simulizi nyengine zinadai kuwa Valentine huenda alinyongwa
kwa kosa la kuwasaidia Wakristo kutoroka katika magereza ya Warumi ambako
walikuwa wakiteswa vibaya.
Inadaiwa kuwa Valentine ndiye aliyetuma maamkizi ya mwanzo
ya mapenzi (valentine) kumpelekea msichana aliyempenda ambaye alikuwa
akimtembelea wakti akiwa gerezani.
Inadaiwa kuwa kabla ya kifo chake, aliandika barua na
kuisaini "Kutoka kwa wako Valentine". Maneno hayo bado yanaendelea
kutumika hadi leo katika kadi za maamkizi ya siku ya Wapendanao.
Kwa upande mwengine, inasadikiwa kuwa kuanzia tarehe 13 hadi
15 Februari, Warumi walikuwa na desturi ya kusherehekea siku iliyojulikana kwa
jina la Lupercalia. Miongoni mwa ada za siku hii ilikuwa ni wanaume kuwapiga
wanawake.
Mnamo karne ya tano, Baba Mtakatifu Gelasius wa Pili,
alikoroga mambo kwa kuichanganya siku ya Mtakatifu Valentine pamoja na ile ya
Lupercalia kwa lengo la kuizika ada hiyo ya kipagani ya Warumi.
Kadiri miaka ilipozidi kusonga mbele ndivyo kadiri siku ya
Wapendanao ilivyozidi kusherehekewa, mpaka ikafikia enzi za Shakespeare na
Chaucer, ambao waliipamba siku hiyo katika kazi zao za sanaa na hivyo kuipatia
siku hii umaarufu zaidi. Katika karne za kati, kadi zilizotengenezwa kwa mikono
ndizo zilikuwa zikitamba.
Hatimaye, utamaduni huo ukavuka bahari na kunigia nchini
Marekani na sehemu nyengine ulimwenguni, na mnamo karne ya 19 mapinduzi ya
viwanda yakachapuza katika uchapishaji wa kadi za maakazi na kuipa umaarufu
mkubwa zaidi siku hiyo. Katika mwaka 1913 shirika la Hallmark likaanza
kuchapisha kadi za Siku ya Wapendao na kubadilisha mkondo wa kihistoria wa
kuadhimisha siku hiyo.
Katika enzi za leo.
Siku ya Wapendao si Sikuu Rasmi nchini Marekani. Watu huenda
makazini kama kawaida, hata hivyo kama zilivyo Siku Kuu nyingi nchini humu,
nayo pia imekumbwa na kimbunga cha biashara tangu pale Hallmark walipoanzisha
kuzalisha kadi zao kwa wingi. Hii ni siku ya pili kwa ukubwa wa mauzo katika
mwaka baada ya siku ya Christmas.
Inakadiriwa kuwa mauzo ya kadi hizo katika siku hiyo hufikia
zaidi ya Dola Billioni 15. Baadhi ya watani wanasema kuwa "iwapo sherehe
za siku ya Wapendanao zitapigwa marufuku nchini Marekani, basi shirika la
Hallmark litafilisika"
Biashara nyengine inayochangamka katika siku hiii ni ya
maua. Tani za maua huuzwa katika siku hii, na baadhi ya wauza-maua huajiri
wafanyazi wa kiasi wiki moja kabla ya siku hii ili kukabiliana na ongezeko la
wateja. Waridi ni nembo ya pili maarufu katika siku hii baada ya ile ya moyo.
Mbali na biashara hizo mbili, kuna zawadi aina kwa aina
ambazo watu huwanunulia wale wawapendao, zikiwemo pipi, chakileti, na vitu
vyengine vya kula na kunywa ambavyo ama hutengenezwa katika umbo la
"moyo" kama ishara ya mapenzi, au kufungwa katika vifurushi vilivyopambwa
katika mfumo kama huo.
Siyo Hallmark tu wanaofaidika katika siku hii, bali biashara
nyingi mauzo yao huongezeka khususan mikahawa ambayo watu wanaotaka kudhirisha
mapenzi kwa wapenzi wao hujazana katika sehemu hizo na kudhihirisha mapenzi ya
hali ya juu kwa kuagizisha milo ya fakhari.
Kwa ujumla Waswahili wanasema "Mtu hujikuna
ajipatapo". Kwa hivyo, kuna wale ambao huwanunulia wapenzi zawadi khafifu
kama vile kadi yenye thamani ya chini, na kendelea mpaka kufikia vito vya
thamani, magari, majumba na sema upendavyo.
Nchini Marekani, Canada na kwengineko, baadhi ya maskuli
huandaa tafrija maalum za Siku ya Wapendanao ambapo wanafunzi hubadilishana
zawadi na marafiki zao ambazo aghlabu huwa ni pipi, chakileti na kadi za
maamkizi.
Wanaosherehekea na Wasiosherehekea siku hii.
Ingawaje siku hii huzalisha mabilioni ya Dola nchini
Marekani, hata hivyo wako watu ambao hawasherehekei siku hii kutokana na sababu
mbalimbali.
Wale wanaosherehekea wanaona kuwa ni siku iliyojaa upendo.
"Siku ya Wapendanao ni siku iliyojaa upendo, anga yote huwa imejaa
mapenzi", anasema Angie Bradlye, Msimamizi wa Uzalishaji katika kiwanda
kimoja nchini Marekani, na kuongeza, "ingawa mume wangu amefariki, lakini
katika siku hii hujihisi kama niko pamoja naye na moyo wangu hujaa furaha"
Naye Mae, anaona kuwa ni fursa kwa wanaume kudhihirisha
mapenzi kwa wapendanao. "Ni siku muhimu kwa wanaume kudhihirisha mapenzi
kwa wanawake wawapendao" alisema.
Kwa upande wa wale wasiosherehekea siku hii nao pia wana
sababu zao.
Scotty ni Mmarekani mwenye asili ya Afrika na anasema
"Mimi siadhimishi siku hii kwa sababu ni siku kuu iliyotengenezwa na
Wazungu tu kwa ajili ya kujipatia pesa kutokana na mauzo ya biashara zao"
Hata hivyo, Blue,ni mwanamke wa Kizungu, lakini hasherehekei
siku hii akisema"Huu ni upuuzi mtupu, si chengine chochote ispokuwa
wanawake wasiokuwa na shukurani kujipatia zawadi wasizostahiki kutoka kwa
mabwana zao"
Wengine huwa hawasherehekei kwa sababu hawana wapenzi wa
kusherehekea nao, kama ambavyo Kendra Simpson kutoka Jimbo la Karolina Ya
Kusini aliiambia Swahillivilla : "Mimi sisherehekei kwa sababu sina mpenzi
kwa sasa, kama nina mpenzi na anapenda kuadhimisha siku hii, basi nitaingia
naye pumbaoni". Hata hivyo alisisitiza kuwa kila siku inapaswa kuwa siku
ya mapenzi kwa wapendao, na siyo siku hii moja tu.
Rai hiyo inaungwa mkono na Bi LaToya Bragg wa jimbo la Ohio,
ambaye anasema "ni jambo la kushangaza kuona watu wanahemkwa na kupoteza
mapesa katika siku hii moja, wakati ambapo mapenzi yanatakiwa kudumu kwa muda
wote ambao watu wapendanao huwa pamoja katika uhai wao"
Athari mbaya za Kijamii.
Bi LaToya aliyeandika kitabu kwa jina "The Heart Of
Me" pia haoni sababu ya kuadhimisha siku hii katika mfumo wake wa sasa kwa
vile unaleta athari mbaya za kijamii. "Kuna watu wengine hali zao za
kiuchumi siyo nzuri, kwa hivyo hawawezi kunnuua zawadi kwa wapenzi wao, na
hivyo wapenzi wanaokosa zawadi kutoka kwa wapenzi wao, hujihisi duni mbele ya
wenzao"
"Aidha huleta athari za kiuchumi kwa watu wenye kipato cha
chini kwa kujikalifisha kuwanunulia wapenzi wao zawadi wazipendazo ambazo
wakati mwnengine ziko nje ya uwezo wao, almradi tu na wao waonekani ni watu
katika jamii"
Mbali na umaarufu wa siku hii, hata hivyo uchunguzi mdogo
uliofanywa na Swahilivilla umeonesha kuwa, idadi kubwa ya watu hawajui asili,
chimbuko na maana ya Siku ya Wapendanao. Kristy, ni afisa wa mapokezi na
usafirishaji katika Shirika moja la vifaa vya magari anasema: "Ninavyojua
siku hii ni ya wanaume kuwanunulia zawadi wapenzi wao, na kwa wanaume siku yao
ni ile inayoitwa 'sweetest hearts day'.."
Naye Amanda Waleker anasema: "Sijui chochote kuhusu
asili ya siku hii, watu wanasherehekea na kuadhimisha, lakini mimi si katika
mambo yangu"
0 comments:
Post a Comment