Utawala wa Aal Khalifa nchini Bahrain unaendelea kukiuka
haki za binadamu hususan za watoto wadogo wa nchi hiyo.
Gazeti la al Akhabari limeripoti habari hiyo na kuongeza
kuwa utawala wa Bahrain unaendelea kuwatia mbaroni na kuwatesa raia wa nchi
hiyo hususan watoto wadogo kwa kisingizio kuwa ni magaidi, licha ya vitendo
hivyo kulaaniwa kimataifa na licha ya kuwa vinapingana na hati ya kimataifa
iliyoidhinishwa na Bahrain yenyewe kuhusu haki za watoto.
Gazeti hilo limeongeza kuwa, kwa mujibu wa takwimu na
taarifa za Taasisi ya Sheria ya Bahrain, zaidi ya watoto 250 wamefungwa katika
jela mbalimbali za nchi hiyo. Wengi wa watoto hao wametiwa nguvuni kwa sababu
za kisiasa na baadhi yao wanasubiri kuhukumiwa kwa sheria eti za kupambana na
ugaidi.
Kituo cha Haki za Binadamu cha Bahrain kimetangaza kuwa
mwezi Novemba mwaka jana, idadi kubwa ya watu waliotiwa mbaroni walikuwa watoto
ambao idadi yao imetajwa kufikia 100.
Hii ni katika hali ambayo taasisi 9 za haki za binadamu
tarehe 20 mwezi Novemba mwaka jana zilitoa taarifa ya pamoja zikieleza kuwa
maafisa wa Bahrain tangu mwaka 2011 hadi hivi sasa wameshauwa watoto zaidi ya
kumi na hivyo kukiuka haki za watoto na wanaendelea kuwashikilia korokoroni
watoto wengine zaidi 1,015 chini ya sheria ya eti kupambana na ugaidi.
0 comments:
Post a Comment