Marekani na Russia zimetangaza mpango wa kukomesha
mivutano yao nchini Syria kuanza jumamosi, kwenye makubaliano ambayo Umoja wa
mataifa umeyataja kuwa ni "dalili ya matumaini" ya kukomesha mgogoro
wa miaka mitano nchi Syria. Hata hivyo makubaliano hayo, ambayo hayahusishi
makundi ya IS, Al Nusra na makundi mengine yaliyoorodheshwa na umoja wa mataifa
kuwa ni makundi ya kigaidi, bado yanasubiri kuidhinishwa na serikali ya Syria
na makundi ya waasi.
Taarifa ya pamoja iliyotolewa na Marekani na Russia
inasema, kundi lolote linalohusika kwenye mgogoro wa Syria litaiarifu Marekani
au Russia utayari wao wa kusimamisha mapambano kabla ya jumamosi. Makubaliano
hayo kuhusu usimamishwaji wa mapambano, ulihimizwa na mkutano wa Munich wa
kundi la uungaji mkono wa Syria ISSG linaloundwa na nchi za umoja wa kiarabu,
Umoja wa Ulaya, Umoja wa mataifa na nchi nyingine 17 ikiwa ni pamoja na China.
Hata hivyo makubaliano hayo yalishindwa kuanza
kutekelezwa kwa muda uliopangwa, kutokana na tofauti kati ya Marekani na Russia
zinazoziunga mkono pande zinazopambana nchini Syria. Utatanishi zaidi umetokea
kutokana na ugumu kwa Marekani kuzishawishi washirika wake wakubwa wa mashariki
ya kati Uturuki na Saudi Arabia, kushiriki kwenye mazungumzo. Saudi Arabia
imekuwa ikitishia kuwa itatuma vikosi vyake kupambana na jeshi la Syria, wakati
Uturuki imeshaanza kuwashambulia wakurd wanaopambana na wapiganaji wa kundi la
IS.
Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Bw Ban Ki Moon
amekaribisha makubaliano hayo, na kuyataja kuwa ni ishara ya matumaini kwa watu
wa Syria, kwamba uchungu walioupata kutokana na vita ya miaka mitano sasa
unakaribia kwisha. Rais Vladmir Putin wa Russia amesema makubaliano hayo ni
hatua halisi kuelekea kukomesha vita, na Rais Barack Obama wa Marekani amesema
kwa sasa kipaumbele ni kwa serikali ya Syria na makundi ya upinzani kutekeleza
makubaliano.
Habari iliyotolewa na vyombo vya habari vya Syria
inasema makubaliano hayo kati ya Marekani na Russia yamekubaliwa na Serikali ya
Syria.
Habari hiyo imenukuu taarifa iliyotolewa na wizara
ya mambo ya nje ya nchi hiyo ikisema, jeshi la serikali litasimamisha
operesheni za kijeshi, lakini litaendelea kupambana na makundi ya kigaidi IS na
Al Qaede.
0 comments:
Post a Comment