RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John
Pombe Magufuli amesema mawaziri ambao hawajajaza Tamko la Rasilimali na Madeni
wawe wamejaza fomu hizo na kuzirejesha katika Ofisi za Sekretarieti ya Maadili
ya Viongozi wa Umma Dar es Salaam ifikapo leo saa 12.00 jioni (Ijumaa, Februari
26, 2016).
Agizo hilo la Rais limetolewa leo na Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa mbele ya waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika ofisini
kwake, Magogoni jijini Dar es Salaam.
“Mheshimiwa Rais ameelekeza mawaziri ambao
hawajajaza tamko la rasilmali au hati ya ahadi ya uadilifu wafanye hivyo na
kuzirejesha kabla saa 12 jioni na Waziri ambaye atashindwa kutekeleza agizo
hili atakuwa amejiondoa mwenyewe kwenye nafasi yake,” amesisitiza Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu amesema wakati akifungua mafunzo ya
Mawaziri na Naibu Waziri kuhusu Mwongozo wa Maadili ya Viongozi wa Umma na
Utekelezaji wa Ahadi ya Uadilifu yaliyofanyika Ikulu jana (Alhamisi, Februari
25, 2016) alikabidhiwa majina ya Mawaziri na Naibu Mawaziri ambao
hawajawasilisha Tamko la Rasilimali na Madeni kwa Kamishna wa Maadili.
Amewataja mawaziri wanaotakiwa kurejesha fomu za
tamko la rasilimali pamoja na hati ya ahadi ya uadilifu kuwa ni Waziri wa Mambo
ya Ndani ya Nchi, Bw. Charles Kitwanga na Waziri wa Nchi (OMR – Muungano na
Mazingira), Bw. January Makamba. Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano
wa Afrika Mashariki, Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa, Dk. Augustine Mahiga
ambaye anatakiwa kurejesha hati ya ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma na
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako ambaye
anatakiwa kutoa tamko la rasilmali na madeni.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nchi (OMR –
Mazingira), Bw. Luhaga Mpina anatakiwa kurejesha fomu za tamko la rasilmali na
madeni pamoja na hati ya ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma.
0 comments:
Post a Comment