Viongozi watano wa nchi za Afrika, wakiongozwa na
Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma, wamewasili Burundi kujaribu kutafuta suluhu
ya mzozo wa kisiasa nchini humo.
Ujumbe huo unaoongozwa unajumuisha marais wa Gabon
Ali Bongo Ondimba, Mauritania Mohamed Ould Abdel Aziz, Senegal Macky Sall na
waziri mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn.
Ziara yao inajiri siku chache tu baada ya Katibu
Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kuzuru taifa hilo na kumhimiza Rais Pierre
Nkurunziza akubali mazungumzo.
Umoja wa Afrika umekuwa ukiishinikiza Burundi kukubali
kushiriki mazungumzo na viongozi wa upinzani ili kumaliza machafuko
yaliyoanza Aprili mwaka jana.
Machafuko hayo yalitokana na hatua ya Rais Pierre
Nkurunziza ya kutangaza kwamba angewania urais kwa muhula wa tatu. Aliwania
baadaye na kushinda.
Hali ilizidishwa na jaribio la mapinduzi ya serikali
mwezi Mei ambalo lilifeli.
Watu zaidi ya 400 wamefariki na maelfu wengine
kutoroka makwao tangu Aprili mwaka jana.
Mwandishi wa BBC aliyeko Bujumbura Prime
Ndikumagenge anasema uwanja mkuu wa ndege wan chi hiyo leo umekuwa na shughuli
nyingi.
Viongozi hao watano wamewasili wakitumia ndege zao
za kibinafsi.
Bw Zuma, kabla ya kuwasili, alituma ndege mbili za
kijeshi za kubeba mizigo ambazo zilikuwa na magari ya kijeshi ya kutumiwa na
maafisa wa kulinda usalama wake.
Viongozi hao, waliolakiwa na mwenyeji wao Rais
Nkurunziza, hawakuhutubu baada ya kuwasili.
Viongozi hao wanatarajiwa kuishinikiza serikali ya
Rais Nkurunziza kukubali mazungumzo yatakayoshirikisha pande zote kwenye mzozo
huo.
Waziri wa mashauri ya kigeni wa Burundi Alain Aime
Nyamitwe amesema serikali hiyo inakubali mazungumzo japo kwa masharti.
0 comments:
Post a Comment