Shirika la Afya Duniani (WHO) limetahadharisha kuwa,
virusi vya Zika huenda vikasambaa zaidi katika siku za usoni kabla ya ugonjwa
huo kupatiwa tiba na kudhibitiwa.
Mkuu wa WHO, Margaret Chan amesema kuna changamoto
kubwa kwa sasa katika juhudi za kudhibiti virusi vya Zika. Amesema changamoto
kuu inatokana na ukweli kwamba mbu wanaosambaza virusi vya Zika wanabadilika
kila mara kitabia na hata kimaumbile. "Hali inaweza kuwa mbaya mno kabla
ya kuboreka" amesema Bi. Margaret Chan.
Mkuu huyo wa WHO ametoa indhari hiyo mjini Rio De
Janeiro, huko Brazil baada ya kukamilisha ziara ya utafiti kuhusu virusi hivyo.
Brazil ndiyo chimbuko la mbu wanaosambaza virusi vya Zika ambavyo kwa sasa
vimeenea katika nchi nyingi duniani.
Virusi hivyo pamoja na mambo mengine husababisha
wanawake wajawazito kujifungua watoto wenye vichwa vidogo na matatizo ya
ubongo. Watu milioni 1.5 nchini Brazil wameambukizwa virusi hivyo na Wizara ya
Afya ya nchi hiyo imesema watoto wasiopungua 580 wamezaliwa na maradhi ya
microcephaly yanaosababishwa na virusi vya Zika.
0 comments:
Post a Comment