WANAFUNZI 1,548 wa Chuo Kikuu cha St. Joseph tawi la
Arusha, wamegoma kuingia darasani kwa siku tatu na kukodi mabasi matatu kwenda
Dar es Salaam kumwona Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce
Ndalichako.
Lengo la safari yao hiyo ya Dar ni kujua hatma yao,
baada ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), kufungia chuo hicho tawi la Songea.
Hata hivyo, Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Yunus
Mgaya, alibainisha kuwa hatma ya chuo hicho, itatolewa rasmi kesho baada ya
tume hiyo kupitia mapendekezo ya tume ya wataalamu iliyoundwa mapema kwa ajili
ya ukaguzi wa chuo hicho, tawi la Arusha.
Kulikuwa na vurugu miongoni mwa wanafunzi juzi
jioni, hali iliyofanya uongozi kufikia uamuzi wa kufunga chuo hicho kwa muda
usiojulikana. Wakizungumza jana kabla ya kuanza safari kwenda Dar es Salaam
kumwona Waziri Ndalichako, wanafunzi hao walisema mmiliki wa St. Joseph ni
mmoja, hivyo kama tawi la Songea lina shida ni wazi matawi yote nchini yana
shida.
Waliomba serikali kutoa ufafanuzi, kabla ya
kuendelea kupoteza fedha za umma walizopatiwa kama mikopo.
“Pamoja na Tume ya Vyuo Vikuu kutoa waraka kwenye
mtandao kuwa kufungwa kwa chuo cha Songea, hakuhusiani na matawi ya chuo hicho,
lakini sisi hatuna hakika tunataka watu hakikishie kama tupo salama,” alisema
mwanafunzi Joel Lameck.
Aliendelea kusema, “na tukimaliza masomo yetu, je,
tutapata ajira serikalini, yasije yakatukuta ya Chuo cha St. John cha Dodoma
ambao hawakupata ajira kwa sababu elimu waliyopata haikuwa na viwango.”
Wanafunzi hao ambao wengi wao hawakutaka majina yao
yatajwe gazetini, walisema wamekuwa wakilalamika mara kwa mara kuwa chuo hicho
kina upungufu mwingi, ikiwemo uhaba wa vifaa vya kufundishia.
Pia wanafunzi hao walihoji sababu za serikali,
kutowaleta wanafunzi wa tawi la Songea iwapo tawi lao la Arusha lipo salama,
badala yake wamepelekwa vyuo vingine, nje ya St Joseph.
Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Siles Balasingh, aliomba
serikali kutoa majibu haraka kwa wanafunzi hao wanaosomea ualimu wa masomo ya
Sayansi, waendelee na masomo yao, kwani wamepata wasiwasi baada ya kufungwa
tawi la Songea, japo hawana shida na chuo.
Alisema wao kama chuo, wamejitahidi kubandika chuoni
hapo tangazo la TCU kwamba tawi hilo halihusiki na matawi mengine, lakini
wanafunzi hawaelewi, wamegoma kuingia darasani, pia wameharibu mali za chuo.
“Hawa wanafunzi leo siku tatu hawataki kuingia
darasani na wamekodi mabasi matatu wanaelekea Dar es Salaam kumwona waziri,
lakini wamewapiga baadhi ya wanafunzi wenzao kwa kuwakataza kufanya mitihani
mpaka wapate uhakika wa masomo tunayowapatia kama tumekidhi vigezo vya mitaala
ya elimu,” alisema.
Alisema walimu wanasikitika kuona vurugu zinatokea
kwa sababu hiyo, hivyo ikiwezekana wanamwomba waziri wa elimu afike chuoni
hapo, kutoa ufafanuzi ili wanafunzi wao hao wapatao 1,518 waendelee na masomo
yao.
Hatma ya chuo kujulikana Ijumaa
Akihojiwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC)
Dar es Salaam jana, Profesa Mgaya alisema mgogoro wa chuo hicho, ulianza muda
mrefu tangu mwaka 2014, hali iliyosababisha tume hiyo kufanya ukaguzi chuoni
hapo.
“Tume iliunda timu ya wakaguzi iliyoongozwa na
maprofesa wa taaluma mbalimbali, waliokagua mfumo wa ufundishaji, mazingira ya
ufundishaji na kuhoji wanafunzi chuoni hapo. Tayari timu hii imewasilisha ripoti
yake kwa TCU,” alisisitiza.
Alisema leo tume hiyo inatarajia kukutana na timu
hiyo na Kamati ya Ithibati majira ya saa 3 asubuhi, kuijadili ripoti ya ukaguzi
wa chuo hicho na saa 9 mchana itaitisha mkutano wa dharura kujadili mapendekezo
ya taarifa hiyo na kutoa maamuzi dhidi ya chuo hicho.
“Tutautangazia umma Ijumaa (kesho) majira ya saa nne
asubuhi kuhusu hatma ya chuo hiki cha St Joseph tawi la Arusha."
0 comments:
Post a Comment