Shirika la Afya Duniani-WHO, limeanzisha kitengo cha
kimataifa kukabiliana na virusi vya Zika, huku likielezea hofu yake kuhusu
ugonjwa huo kwamba unaweza ukaenea hadi barani Afrika na Asia.
Mtaalamu wa Shirika la Afya Duniani-WHO, Dokta
Anthony Costello amesema leo kuwa shirika hilo limeanzisha kitengo maalum ili
kukabiliana na virusi vya Zika, baada ya jana shirika hilo kutangaza kwamba
virusi vya Zika vinavyosababishwa na mbu, kuwa dharura ya kiafya duniani na
wanautaja ugonjwa huo kuwa chanzo cha watoto kuzaliwa na ulemavu na hasa
kuzaliwa na kichwa kidogo pamoja na ubongo ulioathirika katika eneo la Amerika
ya Kusini, ingawa bado hakuna ushahidi wa kutosha kuhusu hilo.
''Asubuhi hii tumeunda kitengo maalum
kitakachowakutanisha pamoja watu wote katika makao makuu ya WHO katika ukanda
huo, ili kukabiliana na ugonjwa huo kwa kutumia mafunzo tuliyoyapata kutokana
na mzozo wa Ebola,'' alisema Dokta Costello.
Shirika hilo liko katika shinikizo la kukabiliana
haraka na virusi vya Zika, baada ya kukiri kuwa iliushughulikia taratibu
ugonjwa wa Ebola uliolikumba eneo la Afrika Magharibi.
Kitengo hicho kujifunza kutokana na Ebola
Costello ambaye ni daktari bingwa wa watoto na
mtaalamu wa matatizo ya watoto wenye vichwa vidogo, amewaambia waandishi wa
habari mjini Geneva kwamba kitengo hicho kipya kilichoundwa kitakuwa na lengo
la kujifunza kutokana na namna walivyoushughulikia mzozo wa Ebola, ili kusaidia
haraka kuutafutia ufumbuzi ugonjwa wa Zika na kasoro zinazowapata watoto ambazo
zinaaminika kusababishwa na virusi vya Zika.
Amesisitiza kuhusu haja ya kuchukuliwa hatua za
haraka akisema hakuna uhakika kwamba virusi vya Zika vitabakia tu kwenye nchi
25 za Amerika ambazo tayari zimetangaza kuwa na visa vya ugonjwa huo. Costello
amesema wana hofu kuwa virusi hivyo vinaweza vikasambaa kwenye maeneo mengine
ya dunia ambako watu wake wanaweza wasiwe na kinga na wanajua kwamba aina ya
mbu wanaoeneza ugonjwa wa Zika, wanapatikana sana kwenye maeneo mengi ya
Afrika, sehemu za kusini mwa Ulaya na maeneo mengi ya Asia, hasa kusini mwa
Asia.
Wakati huo huo, shirika lisilo la kiserikali la
Uholanzi limeanzisha juhudi za kimataifa za kuwapatia wanawake wajawazito
wanaougua ugonjwa wa Zika, vidonge vinavyosababisha mimba kutoka, kwa lengo la
kuzuia uharaka wowote wa wanawake hao kutoa mimba katika njia zisizo salama.
Mkurugenzi wa shirika hilo la wanawake kwenye
mtandao, Rebecca Gomperts amesema wana hofu kuwa virusi hivyo vinaweza kuongeza
utoaji wa mimba usio salama na kwamba wao wanajali sana afya na maisha ya
wanawake, hivyo wanataka kuhakikisha wanawake wanatoa mimba katika mazingira
mazuri ya matibabu.
Virusi vya Zika vinaambukizwa na mbu aina ya Aedes
Aegypti, ambaye pia anaeneza homa ya Dengue na Chikungunya na aligundulika kwa
mara ya kwanza nchini Uganda mwaka 1947.
0 comments:
Post a Comment