Jeshi la Yemen limetangaza kuwa, askari wa serikali kwa
kushirikiana na harakati za kujitolea za wananchi, wamefanikiwa kuwaangamiza
makumi ya askari vamizi wa Saudia na kuwatia mbaroni makumi ya wengine.
Kanali ya televisheni ya Al-Masirah ya Yemen imetangaza
kuwa, jeshi la Yemen na harakati hizo za wananchi zimewaangamiza askari hao
vamizi wa Saudia katika mkoa wa Ma'rib, katikati mwa Yemen na kuwatia mbaroni
wengine zaidi ya 100 katika operesheni hizo. Saudia ilikuwa imewatuma askari
hao ili kuongeza nguvu zake za kijeshi katika mkoa huo, hata hivyo mpango huo
umeishia kufeli. Kwa mujibu wa kanali hiyo, jeshi la serikali nchini Yemen
limewaangamiza askari wengine kadhaa wa Saudia magharibi mwa mkoa wa Ma'rib na
kuteketeza magari yao ya kijeshi. Kadhalika Wayemen wameishambulia kwa
makombora kambi ya jeshi la Saudia ya Sahnul-Jinn, na kuua askari kadhaa wa
nchi hiyo. Kwengineko raia tisa wa Yemen wameuawa na 20 kujeruhiwa leo katika
hujuma ya anga iliyofanywa na ndege za kivita za Saudia katika kijiji cha Bani
Yusuf, magharibi mwa mji mkuu Sana'a.
Saudia kwa kushirikiana na baadhi ya nchi za Kiarabu na
kadhalika Marekani na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, zilianzisha
mashambulizi ya kichokozi dhidi ya Yemen hapo mwezi Machi mwaka jana kwa lengo
la kumrejesha madarakani kwa nguvu rais mtoro na aliyejiuzulu, Abd Rabbuh
Mansur Hadi, njama ambazo hata hivyo hazijafanikiwa kufuatia kusimama imara
wananchi wa taifa hilo.
0 comments:
Post a Comment