SERIKALI imetoa siku saba kwa gazeti la Dira ya Mtanzania
kumuomba radhi Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue na serikali baada ya
kuchapisha taarifa ya uongo na uzushi katika gazeti lao toleo namba 404 la
Februari 29.
Gazeti hilo lilichapisha taarifa yenye kichwa cha habari
kisemacho “Uchafu wa Ombeni Sefue Ikulu” ambayo ni muendelezo wa makala
nyingine kwenye toleo la gazeti hilo la wiki iliyopita.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam
Msemaji wa Serikali Assah Mwambene alisema, endapo gazeti hilo lina ushahidi wa
uchafu huo wapeleke kwenye vyombo vinavyohusika ikiwemo Sekretarieti ya Maadili
na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) vinginevyo hatua
zitachukuliwa dhidi yao ikiwemo kuwapeleka Mahakamani, kufungiwa au
kusimamishwa kuchapisha kwa muda usiofahamika.
Alisema taarifa hiyo ilimtuhumu Katibu Mkuu Kiongozi Ombeni
Sefue kuwa alishawishi juu ya uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu MSD pamoja na kampuni
za CRJE na UGG kupewa zabuni ya kujenga Chuo Kikuu cha Dodoma, Daraja la
Kigamboni na Reli ya Dar es Salaam kwenda Kigali.
Aliongeza kuwa Sefue hakuhusika kwa namna yoyote kushawishi
uteuzi huo kwani ulitekelezwa kwa kufuata kanuni na taratibu zilizowekwa.
“Nafasi hiyo ilitangazwa na bodi Novemba 2013 usaili
ulifanywa na kampuni huru iliyopewa jukumu na bodi na majina matatu yalipelekwa
kwa Rais na Waziri wa Afya hivyo Sefue alikuwa hamjui aliyeteuliwa na wala
hakuwahi kuwa na uhusiano naye alichokifanya yeye ni kutangaza uteuzi baada ya
Rais kuteua, “alisema Mwambene.
Mwambene aliongeza kuwa gazeti hilo pia liliandika uwongo
kuwa MSD haijawahi kuongozwa na Mkurugenzi Mkuu aliye Mfamasia.
“Tangu MSD ianzishwe mwaka 1993 hadi sasa ni Mkurugenzi Mkuu
mmoja tu ndiye aliyewahi kuwa mfamasia sasa mnaona ni jinsi gani wameandika
taarifa ambayo sio ya kweli,” aliongeza.
Aidha alisema taarifa hiyo pia ilimhusisha Sefue na kampuni
ya CRJE lakini suala hilo ni uzushi na uongo kwani wakati kampuni hiyo inapewa
zabuni ya kujenga Chuo cha Dodoma, Sefue hakuwa Katibu Mkuu Kiongozi alikuwa
Balozi wa Tanzania nchini Marekani.
Pia wakati wa mchakato wa kumpata mkandarasi wa daraja la
Kigamboni ulipoanza mwezi Machi 2011 Balozi Sefue hakuwa Katibu Mkuu alikuwa
Balozi wa Tanzania, Umoja wa Mataifa, New York, hata mkataba wa ujenzi wa
daraja hilo kusainiwa Januari 2012 alikuwa ana wiki moja tu katika nafasi ya Katibu
Mkuu Kiongozi.
“Kampuni iliyoshinda tenda (zabuni) wala sio CRJE kama
ilivyoandikwa na gazeti hilo bali ni China Major Bridges Engineering Company
(BCEC) kwa kishirikiana na kampuni ya China Railway Construction (CRCEG)”
aliongeza Mwambene.
0 comments:
Post a Comment