Rais wa Urusi Vladimir Putin ametoa amri
kwa wanajeshi walioko Syria kurejea nyumbani mara moja kwa sababu tayari
wametekeleza asilimia kubwa ya malengo yao.
Akizungumza katika ikulu ya Kremlin
Putin, alisema
''Tayari tumeshakamilisha asilimia kubwa
ya madhumuni yetu nchini Syria kwa hivyo kuanzia jumanne (kesho) ningependa
asilimia kubwa ya jeshi letu kurejea nyumbani.'' alisema bwana Putin.
Tangazo hilo lake limewaacha
wachanganuzi wengi wamepigwa na mshangao kwani hakukuwa na dalili zozote za
kuwepo kwa tukio kama hilo.
Aidha Putin ametangaza hilo katika siku
ambayo mazungumzo ya amani yameanza upya mjini Geneva Uswisi.
Urusi ni mshirika wa karibu sana wa rais
wa Syria Bashar al-Assad.
Ikulu ya Kremlin inasema kuwa rais
Bashar al-Assad alifahamishwa kuhusu hatua hiyo.
Itakumbukwa kuwa kuingia kwa majeshi ya
Urusi katika vita vya Syria vilibadili kabisa taswira ya vita hivyo.
Kwa wakati huo waasi walionekana kuwa
walikuwa wanaelekea kuishinda nguvu jeshi la Syria kinyume na hali ilivyo sasa
ambapo majeshi watiifu kwa rais Assad wameanza hata kuteka maeneo yaliyokuwa
chini ya waasi.
Rais Putin hata hivyo amesema kuwa kambi
ya kijeshi ya Hmeimim na bandari ya Tartus itasalia chini ya jeshi la Urusi.
Huku akisisitiza kuwa zitalindwa ''kwa
hewa ardhini na hata baharini''


0 comments:
Post a Comment