MDHIBITI na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali
(CAG),Profesa Mussa Assad, jana alimkabidhi Rais Dk.John Magufuli taarifa ya
ukaguzi wa hesabu za Serikali ya mwaka 2014/2015, Ikulu Dar es salaam.
Taarifa ya Kaimu Mkurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu,
Gerson Msigwa jana, ilisema Rais Dk. Magufuli alipokea taarifa hiyo yenye
ripoti tano ikiwa ni utaratibu wa katiba
unaomtaka Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali,kukabidhi kwa Rais
taarifa ya ukaguzi kabla ya mwisho wa
Machi.
“Baada ya kupokea taarifa hiyo, Rais Dk. Magufuli
ataikabidhi mbele ya Bunge katika siku saba za mwanzo za kikao kijacho cha
Bunge mjini Dodoma,” alisema Msigwa.
Alisema Rais Dk.Magufuli amempongeza CAG na timu
yake kwa kuandaa taarifa hiyo na ametoa wito kwa chombo hicho kuendelea kufanya
kazi kwa uhuru na ufanisi, huku akiahidi Serikali itatoa ushirikiano wa kutosha
kufanikisha kazi zake.
Itakumbukwa katika Ripoti ya CAG ya mwaka 2014
iliyochunguza kashfa ya Tegeta Escrow, ilizua mjadala bungeni na kusababisha
baadhi ya mawaziri akiwamo wa Nishati na Madini,Profesa Sospeter Muhongo,
kujiuzulu.
Hata hivyo
inaelezwa ripoti ya sasa inaweza kuwa na viporo vya kashfa hizo na
huenda ikafufua viporo vya kashfa zilizopita.
Katika ripoti ya mwaka 2012, Rais mstaafu Jakaya
Kikwete alilazimika kulisuka upya baraza lake la mawaziri baada ya mawaziri
kadhaa kuwajibishwa kutokana na kashfa za ubadhirifu wa fedha za umma.
Mawaziri ambao wizara zao zilibainika kuhusika katika
vitendo vya ubadhirifu wa mali ya umma katika ripoti hiyo na kulazimishwa kujiuzulu ni pamoja na Waziri wa Nishati na
Madini, William Ngeleja.
Wengine ni
Waziri wa Uchukuzi, Omari Nundu, Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo na
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi, George Mkuchika.
Wengine ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel
Maige, Waziri wa Afya na Ustawi wa
Jamii, Dk.Haji Mponda na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk.Cyril Chami.
0 comments:
Post a Comment