SERIKALI imeanza kuwaandaa wafanyabiashara wa ndani
walioko kwenye sekta ya mafuta, jinsi watakavyoweza kuchangia na kunufaika na
fursa mbalimbali zitakazojitokeza katika mradi wa bomba la mafuta ghafi.
Baadhi ya wafanyabiashara hao, leo wanaondoka nchni
wamekwenda kukutana na Rais wa Uganda, Yoweli Museveni pamoja na
wafanyabiashara wa mafuta wa nchi hiyo katika kikao kitakachojadili mradi huo.
Hatua hiyo, imechukuliwa baada ya Kenya kutaka mradi
huo utakaogharimu Dola za Marekani bilioni nne ( zaidi ya Sh trilioni nane),
unaotarajiwa kuanza mapema mwakani kutoka Tanga hadi nchini humo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa
Justine Ntalikwa aliwaambia waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuwa,
Serikali imekutana na wafanyabiashara hao kwa kuwa Tanzania ina asilimia 98 ya
kuupata mradi huo.
“Licha ya mvutano uliopo tumekutana na
wafanyabishara zaidi ya 30, tumewaeleza fursa ambazo zitawanufaisha wao na nchi
kwa ujumla ikiwamo kodi zitakazolipwa, kuongezeka kwa wigo wa ajira na tenda mbalimbali zitakazotolewa wakati na
baada ya kukamilika ujenzi wa mradi huo,”
alisema.
Alisema Tanzania ina kila sababu ya kupata mradi huo
kwa kuwa ina uzoefu wa ujenzi wa mabomba mengine manne na inajivunia Bandari ya
Tanga ambayo ina kina kirefu kuliko bandari zote Afrika Mashariki.
Akizungumzia mvutano uliopo na Kenya kutaka mradi huo, Profesa Ntalikwa
alisema mvutano huo ni suala la dplomasia, tayari mazungumzo kati ya Tanzania
na Kenya yameanza kufanyika ili kuumaliza.
“Tunazungumza na Kenya kwa sababu wao ndiyo wenye
‘due deligence’… kama mnakumbuka mazungumzo ya awali juu ya ujenzi wa bomba
hili yalikuwa kati ya Uganda na Kenya. Tanzania hatukushirikishwa walikubaliana
kuunda kamati iliyohusisha wataalamu wa Kenya na Uganda.
“Kamati hiyo ya watalaam walipanga kutafuta data
(takwimu) wapi patafaa kujengwa mradi huo, walipanga kuanzia kufuatilia data
hizo kuanzia Lamu (Uganda), Mombasa (Kenya) hadi Tanga (Tanzania),” alisema.
Alisema kwa kuwa Tanzania haikushirikishwa katika
makubalino hayo imepanga kupeleka ombi kwa serikali ya Uganda kwamba
haitashiriki kukusanya data hizo huko Lamu badala yake itashiriki kuzitafuta za
Tanga pekee.
Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Sekta ya Mafuta
Tanzania, Dk. Gideon Kaunda alisema wamejipanga kujitoa mhanga na kujidhatiti
kuwekeza katika bishara kwenye mradi huo.
“Tunakwenda Uganda kumshawishi Museveni,
tumejidhatiti na tumejitoa mhanga tutawaeleza kwa nini Tanzania inafaa kuwekeza
mradi huo,” alisema.
Machi 2, mwaka huu, marais John Magufuli na Yoweri
Museveni walikubaliana juu ya ujenzi wa bomba hilo litakalokuwa na urefu wa
kilometa 1,120.
Mradi huo utatoa fursa za ajira kwa watu 15,000 utakapoanza lakini pia uwekezaji huo unalenga
kuongeza pato la taifa na kukuza uchumi wa nchi hizo mbili.
0 comments:
Post a Comment