ALIYEKUWA mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) kwa Mwamvuli wa Ukawa, Edward Lowassa amesema kamwe katika maisha yake, hatasahau
mambo mengi magumu aliyoyapitia.
Amesema pamoja na changamoto zote alizopitia, bado
Mungu ameweza kumsimamia hadi akavuka salama vikwazo vyote.
Amesisitiza kuwa hajakata tamaa na ataendelea
kuwatumikia Watanzania kwa moyo wake wote.
Lowassa alitoa kauli hiyo nyumbani kwake Masaki Dar es Salaam jana, saa chache baada ya Ibada Maalum ya shukrani
iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya
Mashariki na Pwani, Azania Front.
Lowassa ambaye pia ni Waziri Mkuu wa zamani, alisema alipitia mambo mengi
yakiwamo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwaka jana, lakini Mungu alimsaidia na
kumtia moyo.
“Kutokana na magumu mengi niliyopitia sina budi
kutoa shukrani mbele za Mungu. Nilikuwa ninaisubiria sana siku kama ya leo ili
mimi na familia yangu tutoe shukrani
mbele ya Mungu tena kanisani na leo nimetimiza ahadi yangu si kwa uwezo wetu
bali ni kwa neema ya Mungu.
“Wapo Watanzania wengi walioguswa kwa ajili yetu wakiwamo wachungaji, maaskofu,
mapadri na viongozi wa siasa.
“Wote hawa walituwezesha sisi kama familia kufikia
hapa kwa michango yao ikiwa ni pamoja na maombi
hivyo niliona ni vema nijumuike nao katika hafla hii fupi ya shukrani,”
alisema Lowassa.
Lowassa
alisisitiza kuwa Mungu ndiye
kiongozi katika maisha yake hivyo anaamini ataendelea kumwongoza aendelee kuwatumikia Watanzania kwa moyo wake
wote.
Awali akiwa kanisani baada ya kumalizika ibada hiyo,
Lowassa aliwataka Watanzania kusherehekea Sikukuu ya Pasaka kwa amani.
“Sikukuu kama hii tunapaswa kuitumia kuendelea
kuhubiri amani ya nchi yetu…pia tukumbuke suala la Zanzibar ambalo limekuwa
likikwamisha baadhi ya michakato ya maendeleo,”alisema mwanasiasa huyo mwenye
ushawishi mkubwa katika jamii.
Mbowe aiangukia familia ya Lowassa
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mwenyekiti wa
Chadema, Freeman Mbowe aliiomba familia ya mwanasiasa huyo kumruhusu
Lowassa aendelee kuwatumikia wananchi.
Alisema mabadiliko aliyoyafanya Lowassa baada ya
kuhamia vyama vya upinzani kabla ya kuanza
kampeni Agosti mwaka jana, ni makubwa na yameleta nuru ya matumaini kwa
Watanzania.
Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai na Kiongozi wa
Kambi ya Upinzania Bungeni, alisema kwa muda mrefu Watanzania walihitaji
mabadiliko ya fikra na matendo lakini
baadhi yao walikuwa wakiyaongoza kwa woga.
Mbowe alisema uchaguzi si tukio bali ni sehemu ya
mchakato na kwamba kama kuna mtu aliyeangalia uchaguzi kama tukio atakuwa
amekata tamaa.
“Tuna wajibu wa kuendeleza kazi aliyoifanya Lowassa, tunatambua wananchi walipigana sana
kwa ajili ya kufanya mabadiliko na Lowassa alikuwa mshika bendera.
“Sasa kila mmoja kwa nafasi yake awe ndani au nje ya
chama ana wajibu wa kuendeleza
alichokifanya Lowassa.
“Niipongeze familia hii kwa uamuzi wenu
mliouchukua wa kwenda kanisani
kumshukuru Mungu kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza.
“Hiki mlichokifanya kwa familia, marafiki na taifa
kwa ujumla ni jambo la heri na linafaa kuigwa,” alisema Mbowe.
Askofu Lwiza
Awali akizungumza baada ya Ibada ya Jumatatu ya
Pasaka katika Kanisa la Azania Front, Mchungaji Msaidizi wa Kanisa hilo,
Chediel Lwiza alisema hatua ya baadhi ya maaskofu na viongozi wengine kumuunga
mkono Lowassa wakati wa uchaguzi si dhambi na ni suala la utashi.
Alisema maaskofu na watu wengine wakitangaza
kumuunga mkono mwanasiasa kwa jambo lolote ni sawa kwa sababu kuna njia ya siasa na roho.
“Hakuna dhambi yoyote iliyotendeka kwa Askofu
kutangaza kumuunga mkono Lowassa katika siasa, ni haki yake kwa vile Katiba inamruhusu. Pia hata akimuunga mkono
katika roho na katiba bado ana haki,”alisema.
Mchungaji huyo alizungumzia kasi ya Rais John
Magufuli akisema rais anatakiwa kusaidiwa kazi ya utumbuaji majipu ili
asichoke.
“Rais anatakiwa asaidiwe kazi anayoifanya kwa sasa
kwa sababu ni nzito sana, hivyo endapo
akiachiwa peke yake atachoka ndani ya kipindi kifupi,”alisema.
Alisema kitendo cha Magufuli kusimamia misingi ya
haki hana budi atambue kuwa lazima atakuwa na maadui kila sehemu.
“Rais Magufuli anaposema aombewe ni kwa sababu
anakutana na chuki za baadhi ya watendaji ambao hawapendezwi na msimamo
alionao,”alisema.
Askofu Malasusa
Naye Askofu Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na
Pwani, Dk. Alex Malasusa alisema mfululizo wa viongozi kanisani hapo ni ishara
ya umoja na amani kwa kuwa wote ni wakristo.
“Nashukuru kwa wale wote waliokuja kusali kanisani
hapa ingawa si waumini wa kanisa hili, lakini kutokana na tukio la leo (jana)
ndiyo maana wamefika.
“Ni ishara njema kwa kanisa hili kwa vile leo hii…kuna wengine waliokuja ni waislamu
lakini wamevutika na idadi ya viongozi wa Ukawa waliofika,’alisema Askofu
Malasusa.
Alisema
anawapongeza kufika kanisani hapo kama viongozi wa siasa wenye ucha Mungu na kanisa linajivunia
kuwa na viongozi wa namna hiyo.
Askofu Mameo
Akitoa mawazo yake, Askofu wa (KKKT) Dayosisi ya
Morogoro, Paul ole Mameo alisema alifika kanisani hapo kumsindikiza Lowassa ambaye alienda kutoa
shukrani ya pekee kwa yote aliyotendewa na Mungu.
Mameo alisema kila mtu anapaswa kumshukuru Mungu kwa
kila jambo na kitendo alichokifanya
Lowassa kiwahamasishe na wengine kujenga mazoea ya kutoa shukrani za pekee kwa
Mungu.
“Nimekuja hapa kumsindikiza Lowassa, kitendo
alichokifanya kinapaswa kuigwa na kila mmoja wetu, mimi mwaka jana nilifanya
kama hivi….hivyo nawashauri wenzangu nanyi muige mfano huu.
“Mungu wetu ni wa rehema na anamtendea wema kila
mmoja wetu hivyo anapaswa kutolewa shukrani.
“Angalia kuna ajali zinatokea watu wanakatika miguu,
wengine wako hospitalini lakini sisi tupo wazima, Mungu anaendelea
kutupigania,” alisema Askofu Mameo.
Alisema imekuwa ni bahati ya pekee kwa watu wenye
umaarufu na utashi wa siasa kumkumbuka Mungu kwa yale aliyoyatenda.
Meya Mwita
Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita ambaye
pia alihudhuria ibada hiyo na kutambulishwa kwa waumini wa kanisa hilo, aliwashukuru wananchi wa Dar es Salaam kwa
kuiamini Ukawa na kuipa nafasi.
Mbali na familia ya Lowassa pia ibada na hafla hiyo
ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini na siasa wakiwamo Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia,
Meya wa Kiondoni, Boniface Jacob na Meya wa Ilala, Charles Kuyeko.
0 comments:
Post a Comment