KATIKA salamu zake za Pasaka kwa Watanzania, Rais
John Magufuli amewataka Watanzania kuendeleza upendo na mshikamano walionao ili
kuendelea kuilinda amani ya nchi na wasibaguane.
Salamu hizo alizozitoa juzi kwenye Ibada ya Pasaka,
iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) la Azania
Front, Dar es Salaam, ziwe dira na mwongozo mpya kwa Tanzania tuitakayo. Kwa
msisitizo, Rais Magufuli alisema Watanzania wanapaswa kutokubaguana kwa dini,
rangi wala makabila na washirikiane katika umoja wao.
Akaongeza kwamba wakati taifa likiadhimisha sikukuu
hiyo ya kufufuka kwa Yesu Kristo, wananchi wanapaswa kusherehekea kwa kufanya
kazi ili taifa lisonge mbele. Akasema sikukuu hiyo ya kumbukumbu ya kufufuka
kwa Yesu Kristo, Watanzania wafufuke naye katika upendo wake, lakini pia
wahakikishe wanafanya kazi kweli kweli kwa sababu vitabu vinasema ‘asiyefanya
kazi na asile’.
Akabainisha kwamba endapo Watanzania kwa umoja wao,
wakiamua kufanya kazi kwa bidii, Taifa halitakuwa masikini na kuacha kutegemea
misaada ya wahisani wa nje. Tunaungana na Rais katika kauli zake,
zinazosisitiza upendo, mshikamano na bidii ya kazi, kwani vikiwa ndiyo dira ya
nchi, tutasonga mbele na kusahau umasikini uliotesa taifa hili kwa muda mrefu.
Rais Magufuli anasema Tanzania ni nchi iliyojaaliwa
neema kwa kuwa na rasilimali nyingi na hivyo wananchi wanatakiwa kusimama imara
ili iweze kuja kuwa Taifa litakalokuwa likitoa misaada kwa mataifa mengine ya
nje.
Ni ukweli usiopingika kwamba misaada mara nyingi
huambatana na masharti, na nchi hii inao uwezo wa kuwa na bajeti bila kutegemea
misaada, ilimradi watu wake wafanye kazi na waifanye kwa bidii na maarifa.
Uwezo huo tunao, nia ipo na sababu ya kufanya hivyo
tunayo. Rais anaamini Tanzania bila misaada, inawezekana na Watanzania
waliwezeshe hilo. Taifa hili linahitaji kurudisha uzalendo.
Tukane ubinafsi, ufisadi, rushwa, upendeleo, uzembe,
udini, ukabila na mengine ya namna hiyo, ambayo yamelifanya taifa liwe tegemezi
huku rasilimali zikiibwa mchana kweupe kwa ajili ya watu wachache
waliokabidhiwa nyadhifa wakazitumia vibaya kwa faida yao.
Kama salamu alizotoa Rais Magufuli zinafanyiwa kazi,
imani yetu ni kwamba tutaondokana na utegemezi, tutakuwa na bajeti inayotokana
na makusanyo ya ndani na tutaachana na kutegemea mataifa makubwa ambayo nayo
yameendelea kwa sababu ya umoja wao na kuchapa kazi kwa bidii na maarifa.
Rais Magufuli pia akawaomba Watanzania, kutochoka
kuliombea Taifa pamoja na yeye ambaye ana jukumu gumu na zito, lakini kupitia
maombi ya wananchi anaamini atatimiza yale aliyotakiwa kuyatimiza.
Katika hili, tunaamini kila Mtanzania kwa imani
yake, ana wajibu wa kuliombea taifa na Rais Magufuli ili vita anayopigana aweze
kuishinda. Tuungane pia na Askofu Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani,
Dk Alex Malasusa aliyeongoza ibada hiyo ambaye aliwakumbusha wananchi,
kurejesha maadili kwa kumrudia Mungu.
Askofu Malasusa pia akawataka Watanzania kwa imani
zao, kuacha kumsifu Rais Magufuli kwa kupiga makofi na badala yake kila mmoja
kwa imani yake, asimame na kumuombea kwa kuwa sasa taifa limeanza kuwa na
matumaini mapya na nuru kwa kumpata kiongozi aliye mwadilifu. Imani yetu ni
kwamba Watanzania wamesikia na wako tayari kuenzi salamu hizi muhimu ili taifa
liweze kusonga mbele.
0 comments:
Post a Comment