SIKU 15 alizotoa Rais John Magufuli kwa wakuu wa
mikoa, wawe wamejumlisha wafanyakazi wote na kuhakikisha wanaondoa wafanyakazi
hewa, zimetimia leo. Baadhi ya mikoa imeanika idadi ya watumishi hewa,
waliobainika kupitia uhakiki huo, lakini mingi haijafanya hivyo.
Agizo hilo la Rais Magufuli ni sehemu ya maagizo kadhaa
aliyotoa Machi 15 mwaka huu wakati akiwaapisha wakuu hao wa mikoa jijini Dar es
Salaam; ambao aliwasisitiza kuwa ili mradi wamekubali kushika wadhifa huo,
wameingia kwenye mtego.
Pamoja na majukumu mengine waliyopewa kuhakikisha
wanayatekeleza katika uongozi wao, suala la watumishi hewa ni mtego
unaowakabili wakuu hao wa mikoa wakipaswa kujinasua nao ndani ya wiki hii ambao
siku zilizotolewa zimefika ukomo; Vinginevyo, wataweka rehani nyadhifa zao.
Majukumu mengine ambayo wakuu hao wa mikoa walipewa
na Rais wahakikishe wanayatekeleza, ni pamoja na kukabili ujambazi hususan
wakuu wa mikoa ya pembezoni inayokabiliwa na tatizo la utekaji magari kiasi cha
serikali kuamua kuweka utaratibu wa polisi kuyasindikiza.
Mengine ni kukabili watu wazembe, watendaji wanaowanyanyasa
wananchi, njaa, kodi za mazao, migogoro ya ardhi na kuhakikisha wanasimamia
mpango wa elimu bure unafanikiwa.
Tangu Rais atoe maelekezo hayo ya kukabili
wafanyakazi hewa, mikoa mbalimbali inaendelea na mchakato wa kuhakiki
wafanyakazi kwenye idara na taasisi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuwataka
watumishi kuwasilisha nyaraka mbalimbali ikiwemo barua za ajira.
Katika mchakato huo ambao umezaa matunda kwa kubaini
watumishi hewa waliokuwa wakilipwa mishahara, baadhi ya halmashauri zililazimika
kufuta huku baadhi ya halmashauri zimeamuru watumishi wake walio masomoni na
kwenye likizo, warudi mara moja katika vituo vyao vya kazi kuhakikiwa.
Madudu yaibuliwa Miongoni mwa mikoa ambayo imetoa
taarifa za uhakiki ni pamoja na mkoa wa Dodoma, ambao umetajwa kuwa na
watumishi hewa 144. Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana, ameagiza
kupelekewa orodha ya watumishi hao na wakati huo huo kupatiwa maelezo kwa nini
kuna watumishi hewa na kutaka kupatiwa orodha za watumishi hao.
Akizungumza hivi karibuni wakati wa makabidhiano ya
ofisi na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Chiku Gallawa aliyehamia Mkoa wa
Songwe, Rugimbana alisema uhakiki wa watumishi wa serikali umebaini uwepo wa
idadi hiyo ya watumishi hewa .
Mkoa wa Kigoma pia ni miongoni mwa mikoa ambayo
taarifa zake za uhakiki zimeshatolewa ambako imebainika kuwapo watumishi hewa
169 kwa kipindi cha mwaka uliopita.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Emanuel Maganga
amewataka wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wote waliopo katika halmashauri zote
kutaja kiasi cha fedha kilichotumika kulipa mishahara watumishi hewa hao 169
ndani ya kipindi hicho cha mwaka mmoja uliopita.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa huo wa Kigoma, watumishi
hewa waliowabaini, wamo waliokwishafukuzwa, waliofariki na wengine wasiokuwa na
sifa za kuwa watumishi wa umma.
Maganga ametaka fedha walizokuwa wakilipwa watumishi
hao hewa kwa ajili ya mishahara, zirudi na wakati huo huo wakurugenzi wawafute
kwenye orodha ya malipo.
Halmashauri za mkoa wa Kigoma zenye watumishi hewa
na idadi yake kwenye mabano ni Kasulu (78), Kigoma (23), Manispaa ya Kigoma
Ujiji (29), Buhigwe (11), Uvinza (19), Kibondo (5) na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
yenye watumishi hewa wanne.
Halmashauri ya Kakonko ndiyo pekee isiyo na mtumishi
hewa. Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili jana, Mkuu wa Mkoa wa Pwani,
Evarist Ndikilo, alisema leo ambayo ndiyo ukomo wa muda aliotoa Rais, atatoa
taarifa kamili ya kazi hiyo ya kuhakiki wafanyakazi na kuondoa wafanyakazi hewa
watakaokuwa wamebainika.
Ndikilo alisema, ipo timu inayo endelea kufanya
uhakiki kwenye wilaya mbalimbali kwa kushirikiana na wakurugenzi wa
halmashauri. Likizo zaahirishwa Kwa upande wa mkoa wa Dar es Salaam,
Halmashauri ya wilaya ya Temeke ililazimika kuwaita watumishi wake walioko
masomoni na likizo kurudi mara moja katika vituo vyao vya kazi wahakikiwe.
Msemaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Temeke, Joyce
Nsumba alisema hivi karibuni uhakiki uliendelea kwa makundi mbalimbali wakiwemo
watumishi kutoka Idara ya Afya, Elimu, Fedha na Biashara, Kilimo, Mifugo,
Ujenzi na Maendeleo ya Jamii.
Wakati anazungumza na mwandishi wa habari hizi hivi
karibuni, Nsumba alisema walishahakiki watumishi 8,000. Sababu za uhakiki
Uamuzi wa Rais Magufuli kuamuru ufanyike uhakiki, ulitokana na uchunguzi uliofanywa
katika mikoa ya Singida na Dodoma katika halmashauri 14 na kugundulika kwa
watumishi hewa 202 wanaolipwa mishahara.
Aliagiza uhakiki kwa watumishi wote katika wizara,
mikoa, wilaya, idara,taasisi na Wakala za Serikali ndani ya siku 15. “Sasa niwaombe
ndugu zangu wakuu wa mikoa, najua mtakwenda kuwapa maagizo wakurugenzi na wakuu
wa wilaya.
Lakini niwape muda, ndani ya siku 15, wawe
wamejumlisha wafanyakazi wote, wamewatoa wafanyakazi hewa,” ali waagiza. Rais
Magufuli alisema mshahara ujao, ikigundulika kuwapo wafanyakazi hewa kwenye
orodha ya malipo, mkurugenzi husika ajihesabu hana kazi na atafikishwa
mahakamani.
Vile vile amewaambia mawaziri, hususan Waziri wa
Fedha na Mipango aliyekuwapo kwenye hafla hiyo, wakawaeleze watendaji kwenye
wizara zao na taasisi mbalimbali wahakikishe wanawaondoa wafanyakazi hewa ndani
ya siku 15 na wasipotimiza agizo hilo hatua zitakuwa ni zilezile kwani sheria
ni msumeno.
Alisema inasikitisha kuona fedha zinazokusanywa
haziendi kwenye miradi inayopangwa, badala yake sehemu kubwa inatumika kulipa
mishahara ikiwemo hewa. Alisema kwa ujumla Serikali inalipa mishahara kila
mwezi kwa watumishi wake wa umma jumla ya Sh bilioni 549 mpaka bilioni 550.
Alisema kwa hali ilivyo, fedha nyingi zinaishia
kwenye mishahara feki. Nawapa Ma-RC siku 15 mhakikishe Wakurugenzi wa
halmashauri zote wamejumlisha idadi ya wafanyakazi wote waliopo na kuondoa
wafanyakazi hewa katika halmashauri zao,” alisisitiza Rais Magufuli.
Mikoa ya Tanzania Bara ni: Arusha, Dar es Salaam,
Dodoma, Tanga, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe, Rukwa,
Katavi, Kigoma, Kagera, Geita, Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Singida, Tabora,
Pwani, Manyara, Mara, Morogoro na Kilimanjaro
0 comments:
Post a Comment