Shirika la ufadhili la serikali ya Marekani
limesitisha ufadhili wake kwa serikali ya Tanzania likilalamikia matukio kuhusu
uchaguzi wa Zanzibar na kutekelezwa kwa Sheria ya Makosa ya Mtandao.
Bodi ya Shirika la Changamoto za Milenia (MCC)
imesema Tanzania haijatimiza viwango vinavyohitajika ili kunufaika na ufadhili
kutoka kwa shirika hilo, na hivyo basi haitapokea ufadhili wa awamu ya pili
ambao ulikuwa wa jumla ya Dola 472.8 milioni sawa na shilingi trilioni moja za
Tanzania.
Kupitia taarifa, bodi hiyo imesema: "Serikali
ya Tanzania haijachukua hatua za kuhakikisha kuheshimiwa kwa uhuru wa kujieleza
na uhuru wa kujumuika katika utekelezwaji wa Sheria ya Uhalifu wa Mtandao.”
Bodi hiyo aidha imesema Tanzania iliendelea na
uchaguzi wa marudio Zanzibar ambao "haukujumuisha wote na wala haukuakisi
maoni ya wote, licha ya malalamiko kutoka kwa serikali ya Marekani na jamii ya
kimataifa.”
Mabalozi wakosoa uchaguzi wa Zanzibar
Mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Dkt Ali
Mohammed Shein alitangazwa mshindi wa uchaguzi huo uliosusiwa na chama kikuu
cha upinzani, Chama cha Wananchi (CUF).
MCC imesema kwamba huwa inatilia mkazo sana
demokrasia na kujitolea kwa nchi kufanikisha uchaguzi huru na wa haki.
"Uchaguzi uliofanyika Zanzibar na kutekelezwa
nwa Sheria ya Uhalifu wa Mitandao vinaenda kinyume na hili,” imesema.
Tanzania ilipokea Dola 698 milioni katika awamu ya
kwanza.
0 comments:
Post a Comment