SERIKALI ya Marekani kupitia Shirika lake la
Changamoto za Milenia (MCC), imesitisha kuipatia Tanzania msaada wa Dola
milioni 472.8 za Marekani, ambazo ni sawa na takriban Sh trilion moja kwa ajili
ya miradi ya maendeleo kupitia awamu ya pili ya mkataba wa shirika hilo.
Hatua hiyo imetokana na Serikali ya Tanzania
kushindwa kutoa maelezo ya kuridhisha kuhusu kufutwa kwa matokeo ya Uchaguzi
Mkuu wa Zanzibar uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana.
Mbali na hilo, MCC pia ilihitaji kupata uthibitisho
kutoka kwa Serikali ya Tanzania kuhusu Sheria ya Makosa ya Mtandao kutumika
kukwaza uhuru wa kujieleza na kuwakamata watu wakati wa mchakato wa uchaguzi.
Uamuzi huo umekazia taarifa ya awali iliyotolewa
Desemba 16, mwaka jana na Serikali ya Marekani kupitia shirika hilo, ambapo
ilitangaza kusitisha msaada wa dola milioni 472.8 ambazo ni sawa na Sh trilion
moja.
Tamko la MCC
Uamuzi huo ni wazi kuwa umeigharibu Serikali ya
Tanzania kwa kukosa wastani wa Sh trilioni moja za miradi ya maendeleo, baada
ya MCC kuamua kutoshirikiana na Tanzania.
Tamko hilo la MCC kuhusu uamuzi wa Bodi ya
Wakurugenzi kusitisha ubia na Tanzania, lilitolewa jana jijini Dar es Salaam na
Balozi wa Marekani, Mark Childress.
Mara kwa mara na Serikali ya Marekani na Jumuiya ya
Kimataifa zilihoji kuhusu uchaguzi wa marudio wa Machi 20, mwaka huu ambao
walidai kuwa haukuwa jumuishi na wenye uwakilishi stahiki.
“Serikali ya Tanzania haijachukua hatua stahiki
kuhakikisha kuwa uhuru wa kujieleza na kujumuika unalindwa katika utekelezaji wa
Sheria ya Makosa ya Mtandao.
“Mojawapo kati ya vigezo vya msingi kabisa ambavyo
MCC hutumia kuingia ubia na nchi yoyote, ni dhamira ya dhati ya nchi hiyo
kuimarisha demokrasia na kuendesha chaguzi zilizo huru na za haki.
“….uchaguzi visiwani Zanzibar na matumizi ya Sheria
ya Mtandao yanakwenda kinyume kabisa na dhamira hii. Kwa sababu hiyo, wakati ambapo Marekani na
Tanzania wanaendelea kuchangia vipaumbele vingi, Bodi ya Wakurugenzi ya MCC
imeona kwamba Serikali ya Tanzania imekuwa ikichukua hatua zisizoshabihiana na
vigezo vya kupata sifa ya kuingia ubia na MCC,” ilieleza taarifa hiyo.
Kutokana na uamuzi huo, Tanzania inaweza kuathirika
katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo ikiwamo sekta ya miundombinu
kama vile umeme, barabara na maji.
Katika awamu ya kwanza ya fedha za MCC, Tanzania
ilipata dola za Marekani milioni 698 (sawa na Sh trilioni 1.46) ambazo
zilitumika kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya barabara.
Barabara zilizojengwa kupitia fedha hizo za awamu ya
kwanza ni Tunduma- Sumbawanga, Tanga-Horohoro na Namtumbo- Songea- Mbinga.
Desemba 10,
mwaka juzi Marekani pia ilibainisha hatua ya uamuzi wa utolewaji wa
fedha za awamu pili za MCC kwamba utategemea
hatua zitakazochukuliwa na Serikali ya Tanzania kuhusu sakata la
uchotwaji wa fedha zaidi ya Sh bilioni 200 katika akaunti ya Tegeta Escrow.
Kauli ya Serikali
Akizungumzia uamuzi huo, Waziri wa Mambo ya Nje,
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Dk. Augustine
Mahiga, alisema uamuzi huo utawaumiza Watanzania.
Alisema kutokana na hali hiyo bajeti ya mwaka
2016/2017, itaathirika kutokana na uamuzi huo wa MCC kwa Tanzania.
Balozi Mahiga alikiri kuwa uamuzi wa Bodi ya MCC
utaathiri bajeti ijayo ya serikali, kwa kuwa fedha hizo ambazo zingetolewa kwa
kipindi cha miaka mitano zingetumika katika miradi ya nishati ya umeme
vijijini.
Alisema Januari mwaka huu MCC ilitoa taarifa kuwa
misaada ya kawaida inayotolewa kwa ajili ya elimu na afya ambayo ni Sh milioni
700 itaendelea kutolewa kama kawaida kila mwaka.
Alisema kawaida fedha hizo hutolewa kwa nchi
iliyotimiza vigezo vilivyowekwa na Serikali ya Marekani ambavyo ni utawala
bora, uchaguzi huru na haki pamoja na demokrasia isiyo na shaka.
“Hivyo vyote Tanzania imekuwa ikisifika lakini kwa
sababu hii iliyotolewa na Bodi ya MCC kuwa Uchaguzi wa Zanzibar haukuwa huru na
haki na demokrasia haikufuatwa si za
kweli, kwani Tanzania inazingatia masuala hayo kwa mstakabali wa
maendeleo ya Taifa.
“Uamuzi wa Washington tutaadhibiwa wote, Muha wa
Kigoma na Mpemba wa Pemba wote tutaumia. Huo ni uamuzi wao hatuwezi kuingilia,
lakini na yetu hatutaki yaingiliwe.
“Kwa suala la Zanzibar tumejitahidi kueleza pamoja
na kuchukua hatua ya kuimarisha demokrasia na tutaendelea kufanya
hivyo,”alisema Balozi Mahiga.
Wadau wanena
Baadhi ya watu mbalimbali wakiwamo wanasiasa
wamejadili uamuzi wa Bodi ya MCC, huku wakisema kuwa hatua hiyo ni matokeo ya
ubabe wa Serikali.
Kwa upande wake Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe
(ACT-Wazalendo), alisema uzalendo ni kutaka haki ya kidemokrasia Zanzibar.
“Sitakubali kuvishwa koti la uzalendo kwenye suala
la MCC. Hilo ni suala la CCM, kukosa misaada ya Marekani ni matokeo ya ubabe wa
CCM kuhusu Zanzibar.
“Haina mahusiano yoyote na uhuru wa nchi yangu,
nawasihi Wazanzibari wawe na subira Mola kamwe hatawatupa, haki itapatikana tu.
Nawasihi Watanzania kuelewa kwamba CCM ndio imetufikisha hapa na iubebe mzigo
huu bila kufanya ni mzigo wa nchi,” alisema Zitto.
Chama cha ACT-Wazalendo, kimetoa tamko na kusema
kuwa kimepokea kwa masikitiko uamuzi wa Bodi ya Wakurugenzi wa MCC wa kusisitisha
uhusiano na Tanzania.
Makamu Mwenyekiti, Kamati ya Katiba, Sheria na Mambo
ya Nje, Theopister Kumwenda, alisema tangu kuanzishwa kwa MCC kumesaidia miradi
mingi ya maendeleo nchini ikiwemo ujenzi wa barabarani na usambazaji wa umeme
vijijini.
Mtatiro
Naye aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara),
Julius Mtatiro, alisema Tanzania imenyimwa fedha hizo na watakaoumia ni
wananchi.
“Tumenyimwa fedha hizi na watakaoumia ni wananchi.
Kwa hiyo dhambi ya CCM inalipwa na Watanzania wote na kisha viongozi wa CCM
wanaanza kutuhubiria uzalendo.
“Waliopora haki Wazanzibari kwenye masanduku ya
kura, eti pia ulikuwa ni uzalendo,” alisema Mtatiro.
Alisema pamoja na hali hiyo wapo watu wanaoibuka na
hoja ya umuhimu wa kutolilia misaada ya wazungu ambao pia wanatakiwa kujiuliza
kwani misaada ya MCC aliyekwenda kuiomba ni nani.
“Mnapoanzisha hoja ya taifa kujitegemea kiuchumi na
kumnukuu Mwalimu Nyerere, Nkrumah n.k. Tunawauliza swali jingine, ni nani
amekuwa na mamlaka ya kulifanya taifa lijitegemee kiuchumi kwa miaka 50
iliyopita? Si ni nyie nyie?
“…na tena hamtaki kusaidiwa na mawazo mapya hata
baada ya kushindwa na kuendelea kuwalamba miguu wahisani,” alisema.
Magufuli na wahisani
Septemba 29, mwaka jana wakati wa kampeni Rais Dk.
John Magufuli, aliwashangaa watu wanaokejeli safari za nje za Rais mstaafu wa
awamu ya nne, Jakaya Kikwete na kusema kwamba manufaa ya ziara hizo ni makubwa
kuliko wanavyofikiri.
Alisema kupitia safari hizo, Rais Kikwete
amefanikiwa kuwashawishi wafadhili kutoa misaada ya miradi mbalimbali nchini.
Dk. Magufuli alitoa mfano wa Sh bilioni 992
zilizotolewa na Serikali ya Marekani hivi karibuni kupitia mfuko wa MCC kwa
ajili ya miradi ya umeme kama sehemu ya matunda ya safari za Rais Kikwete nchi
za nje.
“Mabilioni yaliyotolewa na MCC, yatasaidia kusambaza
umeme katika mikoa na vijiji vingi nchini na tayari mipango imekamilika ya
kuwafikishia wananchi nishati hiyo,” alisema Rais Magufuli.
0 comments:
Post a Comment