SIKU 15 zilizotolewa na Rais John Magufuli kwa wakuu
wa mikoa kujumlisha waajiriwa wa Serikali wote kwenye mikoa yao, kuwaondoa
wafanyakazi hewa zilikwisha jana huku mikoa michache ikiweka wazi taarifa
kamili kuhusu idadi ya wafanyakazi hao iliyoibaini.
Miongoni mwa mikoa hiyo na idadi ya wafanyakazi hewa
kwenye mabano ni pamoja na Dodoma (144) na Kigoma (169). Mkoa wa Pwani ulikuwa
mbioni kukamilisha uhakiki wake kwa lengo la kutoa taarifa hiyo jana, huku
baadhi ya mikoa ambayo taarifa zake za uhakiki hazijawekwa bayana hadi sasa
ikieleza kuendelea na utekelezaji wa agizo hilo la Rais.
Mikoa hiyo ni pamoja na Dar es Salaam, ambao baadhi
ya wakuu wa wilaya zake wameamuru watumishi wote, hata walio masomoni na
likizo, wawepo kazini ili kuhakikiwa. Rais Magufuli alifikia uamuzi wa
kuwaagiza wakuu hao wa mikoa kuhakiki watumishi kutokana na taarifa aliyoipata
kutoka katika mikoa ya Singida na Dodoma kuwa kuna watumishi hewa.
Inaelezwa kuwa, uchunguzi uliofanywa katika mikoa
hiyo miwili yenye Halmashauri 14, ulionesha kuwa, kuna watumishi hewa 202
wanaoendelea kulipwa mishahara, hivyo kuisababisha Serikali hasara.
Wakati akiwaapisha wakuu hao wa mikoa, Machi 15,
mwaka huu, Rais Magufuli alisema Serikali inatumia Sh bilioni 549 hadi Sh
bilioni 550 kila mwezi kulipa mishahara ya watumishi wa umma. Rais alisema,
inasikitisha kuona fedha zinazokusanywa haziendi kwenye miradi ya maendeleo
inayopangwa, bali huishia kulipa mishahara hewa.
Alionya kuwa, itakapogundulika kuwa kuna mfanyakazi
hewa katika orodha ya wanaostahili kulipwa mshahara mwezi ujao, mkurugenzi
husika ajihesabu kuwa hana kazi, huku akisubiri kufikishwa mahakamani.
Ili kuonesha kuwa alimaanisha alichokisema huku
akitegemea kuona utekelezaji ndani ya muda alioutoa, Rais Magufuli aliwataka
Mawaziri hususan wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango aliyekuwepo wakati
akiwaapisha wakuu hao wa mikoa, awaeleze watendaji kwenye wizara zao na taasisi
mbalimbali wawaondoe watumishi hewa.
Inaelezwa kuwa, watumishi hewa katika mikoa mingi
nchini ni wale ambao majina yao yameendelea kuwepo kwenye orodha ya malipo ya
mishahara, ilhali ikijulikana kuwa wamefariki dunia na wengine kufukuzwa kazi.
Malipo hewa ni hasara kwa taifa, kwa sababu
yanachangia kudumaza maendeleo katika sekta zinazohitaji fedha ili kukua au
kuboreshwa. Baadhi ya sekta hizo ni ya afya na elimu, hasa ikizingatiwa kuwa
wanafunzi wanatakiwa kugharamiwa na Serikali wapate elimu ya msingi hadi
sekondari, ambayo ni ngazi ya kidato cha nne.
Tunawasihi viongozi wa mikoa ambayo taarifa za
uhakiki hazijakamilika hadi sasa kutofanya mzaha ili kumsaidia Rais Magufuli
kuhakikisha mipango yote ya maendeleo ya nchi yetu inafanikiwa. Ikumbukwe kuwa
kuchelewa kutekeleza agizo hilo ni kuendelea kuitia hasara Serikali, kwa kuwa
malipo ya wasio stahili yataendelea kuwepo kwenye orodha isivyo halali na
kulipwa.
0 comments:
Post a Comment