KATIKA kuhakikisha kwamba taifa linapiga hatua kubwa
ya kimaendeleo na wananchi wanapata huduma bora na kwa wakati, Serikali
imeanzisha taasisi mbalimbali za umma ili kurahisisha utendaji na hatimaye
utoaji wa huduma makini kwa wananchi.
Moja ya taasisi hizo ni Taasisi ya Miradi na
Maendeleo ya Miundombinu, (UTT –PID) Hii ni taasisi ya Serikali iliyo chini ya
Wizara ya Fedha ambayo ilianza shughuli zake rasmi Julai Mwaka 2013. Ofisa
Mtendaji Mkuu wa UTTPID Dk Gration Kamugisha anasema kuwa taasisi hiyo
inamilikiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia mia
moja. Anazitaja kazi kuu za UTT-PID kuwa ni utoaji wa huduma za ushauri katika
maeneo ya Upembuzi yakinifu wa miradi mbalimbali, maandalizi ya hadidu za
rejea, mipango ya huduma za kifedha, kuwasilisha miradi na huduma
zinazohusiana.
Msingi wa kuanzishwa kwa taasisi hii na Serikali ni
kuweka manzingira wezeshi ili kupata au kuvutia mtaji binafsi katika kutekeleza
miradi ya maendeleo ambayo sharti iwe inakidhi vigezo vya kuwa na faida za
kijamii, kiuchumi na kifedha. Miradi mingi iliyotekelezwa hadi sasa inahusiana
na uendelezaji wa ardhi na majengo lakini lengo na mtazamo wa taasisi ni zaidi
ya hapo.
Ipo miradi mingi na mikubwa ya kimiundombinu katika
sekta za afya, elimu na nishati, ambayo imeletwa kwenye taasisi na wadau
mbalimbali hasa taasisi za umma ambayo inatafutiwa fedha. Dk Kamugisha
anafafanua kuwa ili taasisi yoyote ile ipige hatua ni lazima iwe na Dira hivyo
kwa upande wao Dira yao ni kuwa mdau wa maendeleo wa kuaminika katika fani ya
Usimamizi wa Miradi na Maendeleo ya Miundombinu na kuwa na mtazamo wa
uwajibikaji wa dhati ili kutosheleza mahitaji kwa wateja na kuendelea kuboresha
huduma.
“Lengo letu ni kuhakikisha kwamba tunawajibika kwa
wateja watu na katika hili ni lazima tutoe huduma bora ambazo zinakata kiu ya
wateja wetu,” anasema. Anabainisha kwamba dhamira yao ni kufungua mitaji
iliyodumaa kwa kuwasaidia wateja kitaalamu katika maeneo ya miradi na maendeleo
ya miundombinu na kuleta ukuaji wa mapato kwa ajili ya wateja na wadau ambao ni
pamoja mwanahisa (serikali).
Anasema wanapokwenda kupanga mji katika eneo lolote
katika nchi yetu kwa mfano, ni wazi kwamba barabara zitachongwa, huduma za
umeme zitafika, huduma za maji zitakuwepo, na shughuli nyingine za kiuchumi
zinazoendana na huduma hizo zitafanyika. “Kwa hiyo utaona ni dhahiri kwamba
wananchi watafaidika na huduma zinazotokana na uwezekezaji wetu katika eneo
husika na hivyo kuchangia ukuaji wa uchumi,” anasema.
Lakini Dk Kamugisha anabainisha kuwa katika
kufanikisha yote hayo ni lazima kuwe na maadili hivyo suala la maadili kwao ni
kipaumbele kikubwa. “Tunaongozwa na misingi ya uwajibikaji, uwezo na motisha
kwa wafanyakazi, uhakika wa ongezeko la wafanyakazi wenye sifa, kuthamini
uvumbuzi, utambuzi na maboresho ili kuepuka au kupunguza uwezekano wa
kujitokeza kwa malalamiko”.
Pia katika kutekeleza majukumu yao anasema suala la
ubora wa huduma ni kipaumbele ambapo dhana nzima ya utoaji bidhaa /huduma zenye
sifa na thamani ya kipekee kwa gharama nafuu. Anabainisha kuwa wamekuwa
wakijitahidi kutoa huduma bora kwa wateja wao katika kuhakikisha kwamba
wanafanya kazi kulingana na thamani ya fedha na hivyo kumridhisha mteja.
“Tunajitahidi sana kukidhi mahitaji ya mteja,
kuhakikisha kwamba taasisi inatoa huduma zilizo bora kwa wateja wao kwa kiwango
kinachokidhi na hata kuzidi matarajio yao,” anasema Dk Kamugisha. Kuhusu suala
la faida anasema taasisi yake imejikimu kimsingi katika uwezo wa kuongeza faida
kutokana na uwekezaji wake kama vile kubadilika kulingana na mazingira ya
kibiashara ili kufikia thamani ya huduma wanayoitarajia wadau wao.
Anaeleza kuwa wanafanya uratibu wa fedha na huduma
zinazohusiana katika maandalizi na mapendekezo ya miradi kwa benki na taasisi
za fedha, utambuzi wa mfadhili/wafadhili wa kifedha, kusaidia katika
uthibitishaji wa nyaraka sahihi na ufatiliaji wa huduma ya mkopo. Tunafanya
kazi ya usimamizi wa siku kwa siku wa miradi ya aina mbalimbali kama ujenzi
upangaji miji, usimamizi wa majengo yaliyokwisha kamilika kwa maana ya kutafuta
na kuhudumia wapangaji.
Usimamizi wa majengo na mali
Dk Kamugisha anasema wanajihusisha pia na utoaji wa
huduma fanisi za usimamizi wa majengo yaliyo chini ya uangalizi thabiti wa
taasisi, ukusanyaji wa kodi ya jengo kwa niaba ya mwekezaji /mwenye jengo. Kwa
mfano mkoani Mbeya taasisi hiyo inasimamia uendeshaji wa Soko la Mwanjelwa
ambalo limejengwa kwa ushirikiano baina ya benki ya CRDB na Halmashauri ya Jiji
la Mbeya.
“Tunalisimamia soko lile vizuri kwa lengo la
kuhakikisha kwamba wananchi ambao ndiyo walengwa wanapata huduma bora na hivyo
kusaidia katika kunyanyua hali zao za maisha na pia wakati huo huo kuhakikisha
kwamba Halmashauri ya Jiji inatimizia malengo yake,” anasema. Anasema kuwa
UTT-PID, daima inashawishika kutoa huduma nyingine yoyote hususani katika
upande wa miundombinu na uwekezaji katika sekta zote za kiuchumi.
Mafanikio ya taasisi mpaka sasa Anasema kuwa
wamefanikiwa katika kuwezesha utekelezaji wa mradi wa Shirikisho la Vyama Vya
ushirika Tanzania (TFC) Taasisi iliwezesha upatikanaji wa mtaji ambao ulitumika
katika ujenzi wa jengo jipya la ghorofa 20 na ukarabati wa jengo la zamani. Pia
kwa upangaji wa miji katika mkoa wa Lindi jumla ya viwanja 10,000 vya matumizi
mbalimbali vinatarajiwa kupimwa.
Hadi sasa jumla ya viwanja 2,473 vimeshapimwa (awamu
ya kwanza) kwa ufadhili wa Taasisi yetu ikishirikiana na Halmashauri ya
Manispaa ya Lindi na wadau wengine wa maendeleo mkoani humo. Viwanja hivyo
viliuzwa kwa utaratibu wa wazi kabisa kwa wateja mbalimbali kupitia Benki ya
Posta.
“Ilikuwa haijawahi kutokea kwa Halmashauri ya
Manispaa ya Lindi kupima viwanja vingi namna hii kwa wakati mmoja. Pamoja na
viwanja hivi kuonekana ni vingi bado kuna wananchi waliokosa . Hii inaonesha
jinsi ambavyo wananchi wanatamani kuishi katika maeneo yaliyopimwa na
kupangiliwa vizuri,” anafafanua Dk Kamugisha. Anasema kuwa katika Wilaya ya
Sengerema mkoa wa Mwanza awamu ya kwanza katika Mradi huu taasisi kwa
kushirikiana na Halmashauri iliwezesha upimaji wa viwanja 1,230 na uwekezaji wa
baadhi ya miundombinu.
Kwa kushirikiana na Manispaa ya Bukoba, taasisi
imefanikiwa upimaji wa viwanja karibu 5000. Kwa mujibu wa taarifa za ndani ya
Manispaa ya Bukoba, viwanja vilivyopimwa kwa ufadhili wa UTT-PID kwa wakati
mmoja ni vingi kuliko viwanja vyote vilivyokuwa vimewahi kupimwa ndani ya
manispaa hiyo tangu uhuru.
Kuhusu manufaa ya miradi hiyo, Dk Kamugisha anasema
kwamba manufaa ni makubwa sana mathalani katika mkoa wa Lindi, utekelezaji wa
mradi wa upimaji viwanja uliiwezesha Halmashauri ya Manispaa ya kutekeleza
miradi mbalimbali kutokana na fedha zilizopatikana kwenye mradi huo.
“Maabara zimejengwa katika shule za sekondari nyumba
za walimu, boti inayotoa huduma kwa wananchi kati ya Lindi mjini na eneo la
Kitunda,” anasema. Mradi huo umekuza shughuli za kiuchumi katika maeneo
uliyoyapitia, mathalani, wa miundombinu kama vile ya barabara. “Hali hiyo
imesababisha hata uchumi wa mwananchi mmoja mmoja kukua kwakuwa wanaweza
kufanya shughuli mbalimbali za kimaendeleo sanjari na mradi huo,” anafafanua.
Lakini pia faida nyingine ya miradi yao ya kupanga
miji ni upatikanaji wa hati kwa wanunuzi ndani ya muda mfupi. “Utaona sasa
wananchi wanaweza kupata huduma mbalimbali za kifedha kupitia hati hizo na
hatimaye kujiletea maendeleo,” anasema. Baadhi ya wananchi wanaipongeza UTT-PID
kwa kuendesha miradi mbalimbali ya upimaji ardhi na kiuchumi kwa ujumla kwani
inachochea ukuaji wa uchumi.
“Mimi kwa kweli nawapongeza hasa kwa kupima viwanja
kwani wamekuwa wakiwasaidia Watanzania hasa wale wa hali ya chini kuweza kupata
hati ambazo zinawasaidia katika shughuli zao mbalimbali za kiuchumi,” anasema
John Mwakatobe mkazi wa Gongo la Mboto, Ilala jijini Dar es Salaam. Anafafanua
kuwa si rahisi kwa kila mtu hata kama ana fedha kuweza kufatilia hati kiwanja
katika mamlaka husika kwa muda muafaka, lakini kwa kuwatumia taasisi ya UTT-PID
ni jambo linalofanyika kwa muda mfupi sana.
Naye Ali Salehe, mfanyabiashara eneo la Mnazi Mmoja
anawapongeza UTT-PID kwa kukarabati jengo la zamani la Ushirika na kujenga jengo
jipya la kisasa ambalo limesaidia kuupendezesha mji. “Nawapongeza sana kwa
kuupendezesha mji pamoja na kujenga jengo la kisasa eneo hilo ambalo lina
shughuli nyingi za kiuchumi jambo ambalo linasaidia kukuza uchumi wa nchi kwa
kuiingizia serikali mapato,” anasema.
0 comments:
Post a Comment