SIKU mbili tangu kufanyika kwa uchaguzi wa marudio
Zanzibar, na siku moja kabla ya kuapishwa Dk Ali Mohamed Shein, Maalim Seif
Shariff Hamad, Mgombea wa Urais wa Zanzibar katika uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka
jana kupitia Chama cha Wananchi (CUF), amesema CUF haitashiriki uchaguzi wowote
chini ya Tume ya Jecha Salim Jecha.
....Anaandika Josephat Isango....
Akizungumza akiwa Hoteli ya Serena ambapo yupo kwa
mapumziko baada ya kulazwa, Maalim Seif amesema kuwa kama yatatokea maridhiano
yatakaoongozwa na kusimamiwa na taasisi huru za kidemokrasia, bila vitisho vya
majeshi na polisi, kuwa na vyombo huru vya habari na tume huru sio hii iliyopo
Zanzibar chini ya Jecha, hapo CUF kitaweza kufikiri kushiriki uchaguzi.
Ameongeza kuwa harakati za kudai haki, zitaendelea
kwa njia ya amani ili marekebisho ya tume yafanyike kwani kwa utaratibu uliopo
hata mwaka 2020 upinzani ukishinda Tanzania bara, Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kitang’gang’ania madaraka.
“CUF tunaamini katika amani, tusichafue amani,
tusichafue nchi yetu, tuendeleze mapambano kwa kutoitambua serikali iliyojiweka
madarakani katika uchaguzi haramu wa Machi 20 mwaka huu, wala hatutaipatia
ushirikiano wowote katika mambo yote” alisema.
Uchaguzi wa 20 Machi, sio halali. Jecha hakuwa na
uwezo wa kisheria wala kikatiba kufuta uchaguzi, mgogoro uliopo sasa
umesababishwa na Jecha, ukapewa baraka za CCM, sababu CCM hawataki kushindwa,
na hawataki wapinzani kuongoza. Kila CCM ikishindwa hutoa visingizio.
“Kabla Kikwete (Rais Mstaafu Jakaya Kikwete)
hajaondoka madarakani, aliniambia kuwa Maalim CCM wanakuogopa, wanajua
ukishinda utaweza kuvunja Muungano, lakini nilimwambia, CCM ndio wenye jeshi,
wenyewe ndio wenye dola mimi nitavunjaje Muungano? Hiyo ni hofu na visingizio
tu ili waendelee kukwapua madaraka.”Alisema.
Ameweka bayana kuwa kwa sasa CCM imewarejesha
wananchi miaka 20 iliyopita, kwani uhasama wa watu kutengana kwenye shughuli za
kijamii kwa sababu za tofauti za kisiasa zimeanza kurejea baada ya CCM
kulazimisha kukwapua madaraka ya wananchi kwa kufuta uchaguzi wa 25 Oktoba
mwaka jana.
Akizungumzia suala la Muungano kama ambavyo amekuwa
akihusishwa Maalim seif amesema kuwa sasa Muungano utavunjwa na CCM, sio CUF
wala yeye kama wanavyosingizia.
Ameongeza kuwa kwa sababu CCM ya bara ndio
inalazimisha kuweka viongozi waliokataliwa na wananchi wa Zanzibar na chama
chao kwa kutumia majeshi na polisi wao ndio husababisha wananchi wachukie
Muungano.
Aidha kuhusu uchaguzi wa marudio wa Machi 20, Seif
amesema kuwa CUF imeshinda, kwani wananchi wa Zanzibar waliitikia wito wa CUF,
wakasusa, hawakujitokeza kupiga kura. Hizo zilizotangazwa na Tume ya Uchaguzi
ya Zanzibar (ZEC) wanajua walipozipata wao na CCM.
“Mimi nilishasema tangu awali, kuwa matokeo
yameshajulikana kabla ya uchaguzi, sababu ni ya kupika, namhurumia Dk Shein kwa
kujisifu kupata kura ambazo hazipo, mawakala waliweka wao na wasimamizi na kuna
taarifa kuwa wapigakura walikuwa wanapewa rundo la kura, wapige na kutumbukiza
ili kukidhi matakwa ya CCM.” Amesema Maalim Seif.
Maalim Seif amewatakia utulivu Wazanzibar wote, na
kuwaarifu kuwa afya yake ni imara, na atarejea Zanzibar wakati wowote kuungana
nao.
Chanzo:MwanaHALISI Online.
0 comments:
Post a Comment