RAIS wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk.
Billy Haonga ameitaka Serikali ieleze ukweli kuhusu ukosefu wa vifaa tiba na
dawa katika hospitali mbalimbali.
Pia ameitaka kueleza namna ya kutatua changamoto
nyingine zinazokabili sekta ya afya na si kuaminisha umma kuwa watoa huduma
ndiyo tatizo.
Kauli hiyo ameitoa
jijini Dar es Salaam jana,wakati akizungumza na waandishi wa habari
baada ya tukio lililotokea juzi lililomhusisha Dk, Dickson Sahihi wa Hospitali
ya Rufaa ya Ligula, mkoani Mtwara
kupigwa, kudhalilishwa utu kwa kuvuliwa nguo na ndugu wa wagonjwa.
Alisema sekta ya afya ni moja ya sekta zenye
matatizo makubwa ya rasilimali watu, vifaa na dawa na mpaka sasa inafanyakazi
chini ya asilimia 50 katika maeneo mbalimbali nchini.
“Daktari mmoja, anahudumia wagonjwa kati ya 25,000
hadi 30,000 maeneo ya mjini, kule
vijijini ni kati ya 50,000 hadi 100,000 tofauti na mpango wa Shirika la Afya
Duniani (WHO), linataka daktari mmoja
kuhudumia wagonjwa wasiozidi 10,000 katika miji inayoendelea ,” alisema Haonga.
Alisema kwa
upande wa dawa hali ni mbaya zaidi, huku
maeneo mengine yakikosa dawa wiki za mwanzo za mwezi na baada ya hapo
hazipatikani kabisa.
Kutokana na hali hiyo, ametoa siku 14 kwa Serikali
kuchukua hatua stahiki kwa vitendo na kama haitafanya hivyo chama hicho kitaitisha mkutano mkuu wa
dharura kujadili usalama wao.
“Mbali na kupigwa Dk.Dickson, matukio mengine ambayo
yametuhuzunisha ni pamoja na kusimamishwa hadharani kwa wafanyakazi madaktari
na manesi kutokana na uduni wa huduma unaosababishwa na upungufu na ukosefu wa
vifaa tiba.
“Kuzingirwa nyumba ya daktari mkoani Katavi na ndugu
wa wagonjwa kwa lengo la kumdhuru, baada ya mgonjwa wao kufariki dunia kwa
ukosefu wa dawa na damu, haya yote ni matukio ya kusikitisha,”alisema Haonga.
Juzi Serikali ililaani kitendo cha kupigwa daktari
huyo na kuviagiza vyombo vya dola kuwachukulia hatua wahusika wote.
Kauli hiyo,
ilitolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.
“Ninawasihi sana wananchi wanaopatiwa huduma katika
vituo vyetu vya afya kote nchini, kuacha mara moja tabia ya kujichukulia sheria
mikononi na kufanya vitendo vinavyoweza kuwakwaza watumishi wa afya,” alisema
Ummy.
0 comments:
Post a Comment