RAIS Dk. John Magufuli, ameanika madudu aliyoyakuta
ndani ya Serikali ikiwemo mmoja wa mfanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA), kulipwa mishahara ya watu 17 na kuagiza mfanyakazi huyo afikishwe
mahakamani.
Pamoja na hali hiyo amesema wapo watumishi
wanaolipwa mishahara mikubwa ambayo inafikia hadi Sh milioni 40 kwa mwezi
ambayo sasa itapunguzwa na kuweka kima
cha juu cha mshahara usiozidi Sh milioni 15.
Rais Magufuli alitoa taarifa hiyo jana nyumbani
kwake katika Kijiji cha Mlimani, Wilaya ya Chato mkoani Geita ambapo alihutubia
kwa mara ya kwanza tangu achaguliwe kuwa Rais.
Dk. Magufuli alisema Serikali yake imejiandaa
kuboresha maslahi ya wafanyakazi kwa kupunguza kodi kutoka asilimia 11 ya sasa
hadi asilimia 10 au 9 kuanzia bajeti ijayo.
“Kuhusu tatizo la wafanyakazi hewa, uhakiki mdogo
uliofanywa hivi karibuni, umebaini wafanyakazi hewa 1,680 waliokuwa wakilipwa
shilingi bilioni 1 na milioni 800 na kwamba ni matarajio kuwa uhakiki
unaofanywa nchi nzima utaisaidia Serikali kubaini wafanyakazi hewa wengi zaidi
na kunusuru fedha nyingi zaidi za Watanzania.
“ Leo (jana) hii yupo mfanyakazi mmoja wa Mamlaka ya
Mapato TRA ambaye alikuwa akilipwa mishahara ya watu 17 na huyo ni lazima
afikishwe mahakamani.
“…serikali imejiandaa kuboresha maslahi ya
wafanyakazi kwa kupunguza kodi kutoka asilimia 11 ya sasa hadi asilimia 10 au 9
kuanzia bajeti ijayo, lakini kwa wale wanaolipwa mishahara mikubwa ambayo
inafikia hadi shilingi milioni 40, itapunguzwa na kuweka kima cha juu cha
mshahara usiozidi shilingi milioni 15,” alisema Rais Magufuli.
Alisema anashangazwa na hatua ya baadhi ya watu
kuishi kama malaika huku wengine wakiishi kama masheteni, jambo ambalo halina
nafasi katika Serikali yake.
“Nyiye mliokuwa mnaishi kama malaika, sasa zamu yenu
kuishi kama mashetani,” alisema Dk. Magufuli huku akishangiliwa na umati wa
wananchi waliohudhuria katika mkutano huo.
Misaada ya wafadhili
Pamoja na hali hiyo Rais Magufuli, amewataka
Watanzania kuchapa kazi kwa juhudi ili nchi iondokane na utegemezi wa misaada
ya wafadhili ambayo huandamana na masharti.
Alisema jukumu kubwa lililo mbele kwa sasa ni
kushikamana na kujisimamia katika maendeleo ili kila mmoja ahakikishe anaongeza
uzalishaji na utendaji kazi mahali pake pa kazi.
“Kwa hiyo ni lazima tujisimamie sisi wenyewe na
tukijisimamia sisi wenyewe kwa kila mmoja kuwajibika mahali alipo, kama ni
mfanyakazi afanye kazi kwelikweli, kama ni mkulima afanye ukulima wake
kwelikweli, kama ni mfanyabiashara afanye biashara kweli kweli, kama ni mfugaji
afuge kwelikweli, kama ni mvuvi avue kwelikweli, Tanzania hii tutavuka,” alisema
Rais Magufuli.
Alisema Serikali yake imeamua kuchukua hatua
kudhibiti nidhamu serikalini, kwa kuhakikisha inawachukulia hatua watumishi wa
umma wanaolisababishia taifa upotevu mkubwa wa fedha, na ameahidi kuwa hatua
hizo maarufu kwa jina la ‘Kutumbua Majipu’ zitaendelea kuchukuliwa hadi tatizo
hilo likomeshwe.
Onyo kwa wateule
Pamoja na hali hiyo Rais Magufuli amewakumbusha
viongozi wote wakiwemo wakuu wa mikoa, wilaya, makatibu tawala na wakurugenzi,
kutekeleza wajibu wao ipasavyo na ameweka bayana kuwa mahali popote ambapo
hapatakuwa na ufanisi, kiongozi husika atakuwa amedhihirisha kuwa hatoshi
kuendelea na wadhifa aliopewa.
Rais Magufuli, aliwapongeza walimu kote nchini kwa
kufanya kazi nzuri ya kufundisha, licha ya changamoto ya ongezeko kubwa la wanafunzi
waliojiunga darasa la kwanza mwaka huu,
ambapo aliwataka lwazazi na kamati za shule kushirikiana na walimu
kuwasimamia wanafunzi ili waweze kufanya vizuri katika masomo yao.
“Niziombe kamati za shule zote Tanzania nzima, kama
haziwezi kusimamia nidhamu ya wanafunzi shuleni, zile kamati za shule
zijiuzulu.
“Lakini pia kama wewe ni mwalimu mkuu, shule yako
kila siku inatoa divisheni ziro nyingi kila mwaka, sioni sababu ya wewe
kuendelea kuwa mwalimu mkuu,” alisema Dk. Magufuli.
0 comments:
Post a Comment