WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa
Makame Mbarawa, ametoa mwezi mmoja kwa watu na taasisi zilizokopa nyumba za
Serikali kulipa. Mbarawa aliyasema hayo jana Dar es Salaam wakati akizungumza
na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).
Alisema anataka fedha hizo zilipwe haraka,
vinginevyo atawataja katika vyombo vya habari watakaoshindwa kukamilisha madeni
yao na kuagiza waondoke kwenye nyumba hizo. “Kama ni watu binafsi au taasisi za
Serikali ni lazima walipe ili na sisi tuendelee kufanya kazi zetu vizuri.
Naomba mlisimamie hilo na fedha hizo zilipwe,”
Mbarawa alisema. Aliongeza kuwa huu ni wakati wa kufanya kazi kwa kasi
inayostahili. Profesa Mbarawa alisema pia kuwa ufisadi katika wizara hiyo sasa
ni mwiko. Alisema kuwa ufisadi hauangalii ukubwa wala udogo hivyo kwake uwe
mdogo au mkubwa ni ufisadi tu.
“Ninajua na ninyi TBA mna kashfa zenu. Ninawaambia
tutapambana na wajanja wajanja wote kwa sababu hatutaki tufike katika majipu,”
alisema. Aidha, aliwataka wafanyakazi wa wakala huo kufanya kazi kwa weledi na
kuacha kufika ofisini ‘kuchati’ katika mitandao ya kijamii na kuondoka, badala
ya kufanya kazi.
Wakati huo huo, alitoa onyo kwa wanaotumia namba
zake za simu kufanya utapeli na kusema atawachukulia hatua za kisheria.


0 comments:
Post a Comment