BODI ya Sukari Tanzania imeshusha bei ya sukari kwa
kutangaza bei elekezi, inayoonesha bidhaa hiyo kuanzia sasa inauzwa Sh 1,800
kwa kilo nchini kote. Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi, Henry Simwanza alisema, wafanyabiashara wote wanapaswa
kuzingatia agizo hilo.
Aidha alisisitiza wafanyabiashara kuhakikisha kuwa
sukari inaendelea kusambazwa na kuuzwa kwa wananchi bila kuihodhi. Awali, juzi
alipozungumza na waandishi wa habari, Simwanza alisema bei elekezi ya sukari
ilikuwa Sh 2,000 kwa Dar es Salaam na miji jirani.
Kwa upande wa mikoa iliyo pembezoni, bei ilielekezwa
iwe 2,200. Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema juzi
wakati akisisitiza bei elekezi hiyo (ya awali), kulikuwa na kikao kingine
kikiendelea kujadili suala la sukari, ambacho ndicho kilifikia uamuzi wa bei ya
Sh 1,800 baada ya kujiridhisha.
“Kuhodhi bidhaa ni kuhujumu uchumi wa nchi, sukari
ni bidhaa nyeti inayohitajika sana. Tunawataka wafanyabiashara wote watii agizo
hili,” alisema Simwanza. Alisema maofisa wa bodi ya sukari Tanzania, kwa
kushirikiana na mamlaka nyingine za serikali, hususani maofisa biashara wa
mikoa na wilaya watafuatilia na kusimamia utekelezaji wa agizo hilo la bei
elekezi.
“Serikali ikisema kitu ni amri. Niseme tu hatutasita
kuchukua hatua stahiki za kisheria kwa wale watakaobainika kupandisha bei au
kuhodhi bidhaa hiyo,” alisema Simwanza. Juzi Simwanza akizungumza na vyombo vya
habari alisema upatikanaji wa sukari nchini ni wa kuridhisha na ipo akiba ya
kutosheleza nchi nzima.
Alisema pamoja na baadhi ya viwanda kusimamisha
uzalishaji wa sukari kutokana na msimu kuisha, hali ya bidhaa hiyo nchini ni
nzuri na ipo zaidi ya tani 62,000. Aliwataka wasambazaji wakubwa wa sukari
hususani kampuni ya Alneen Enterprise ya jijii Dar es Salaam , ambayo
imethibitisha kuwa na sukari tani 8,600, waitoe na kuiuza.
Wakati huo huo, Waziri wa Viwanda, Biashara na
Uwezeshaji, Charles Mwijage alisisitiza kuwa hakuna uhaba wa sukari nchini na
kuwataka wafanyabiashara walio na leseni za kuingiza na kuuza bidhaa hiyo,
kutoificha.
Mwijage alitaka watu wenye taarifa juu ya
mfanyabiashara aliyefungia sukari katika ghala lake ampelekee, afunge ghala
husika mara moja. Alisema serikali inajikita zaidi katika uanzishaji wa viwanda
vya sukari na kuongeza ajira na si katika kuagiza sukari kutoka nje.
Miongoni mwa jitihada hizo ni pamoja na mazungumzo
inayofanya na mwekezaji anayetaka kuwekeza katika ujenzi wa kiwanda cha sukari
mkoani Kigoma, atakayewasili nchini wakati wowote kukamilisha taratibu.


0 comments:
Post a Comment