Rais wa Marekani Barack Obama ameeleza matumaini
yake kwamba hali ya Cuba itaimarika, kwenye hotuba iliyopeperushwa moja kwa
moja kupitia runinga.
Kiongozi huyo wa Marekani, ambaye ndiye wa kwanza
kuzuru Cuba akiwa bado madarakani katika kipindi cha miaka 88, alitoa hotuba
hiyo kutoka ukumbi wa Grand Theatre mjini Havana.
Bw Obama alisema alifika Cuba “kuzika masalio ya
Vita Baridi” na miongo mingi ya uhasama.
Alimwambia Rais wa Cuba Raul Castro kwamba hafai
kuiogopa Marekani na pia hafai kuogopa “usemi wa watu wa Cuba”.
Bw Obama alisema wakati umefika kwa Marekani na Cuba
kuacha nyuma yaliyopita na kusonga mbele “kama marafiki na majirani na kama
familia, pamoja” kwa siku za usoni zenye ufanisi.
Amewataka raia wa Cuba kuacha nyuma vita vya
kifalsafa na kujieleza sio kwa kupinga Marekani bali kwa kujieleza wao binafsi
ama raia wa Cuba.
"Licha ya siasa hizi zote, watu ni wale wale na
Wacuba ni Wacuba,” alisema.
Aidha, amehimiza kuondolewa kwa vikwazo vya
kibiashara vilivyowekewa nchi hiyo na Marekani miaka 54 iliyopita. Tamko hilo
lilishangiliwa sana na raia wa Cuba.
Ni Bunge la Congress pekee linaloweza kuidhinisha
kuondolewa kwa vikwazo hivyo.
Bw Obama alikamilisha ziara yake ya siku tatu kwa
kuungana na Rais Castro kutazama mechi ya besiboli uwanja wa Latinoamericano
mjini Havana.
Baada ya kuondoka Cuba, Bw Obama ameelekea Argentina
siku ambayo inalingana na maadhimisho ya miaka 40 tangu kutokea kwa mapinduzi
yaliyoingiza mamlakani utawala dhalimu wa kijeshi.
Baadhi ya makundi yanapanga maandamano kushutumu
Marekani ambayo inadaiwa kusaidia jeshi wakati wa mapinduzi hayo ya 1976.
0 comments:
Post a Comment