Kufuatia Mabadiliko ya Wajumbe kwenye Kamati za
Kudumu za Bunge yaliyofanywa na Mhe. Job Ndugai (Mb) Spika wa Bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania jana tarehe 22 Machi, 2016; baadhi ya Vyombo vya Habari
na Mitandao ya Kijamii imenukuliwa ikihusisha mabadiliko hayo kuwa yamefanywa
kutokana na tuhuma za rushwa kwa baadhi ya Kamati za Bunge kufuatia ripoti ya
chombo kimoja cha Habari.
Ofisi ya Bunge inapenda kutoa ufafanuzi kuwa madai
hayo hayana ukweli wowote, bali mabadiliko yaliyofanywa na Mhe. Spika ni ya
kawaida na wala hayakuanisha dosari zozote katika Utendaji wa kamati za Kudumu
za Bunge. Msingi wa Mabadiliko ya Wajumbe kwenye kamati, umelenga kuzingatia
mahitaji mapya na changamoto zilizojitokeza baada ya kuunda Kamati hizo mwezi
Januari 2016 ambapo alikuwa ameanza kufanyia kazi mabadiliko hayo tangu mapema
mwezi huu.
Waheshimiwa Wabunge wanaosakamwa kwa uvunjifu wa
Maadili kupitia Mitandao ya kijamii na Magazeti, ni budi wakatendewa haki kwa
sababu Mhe. Spika anazingatia sana Utawala wa Sheria na kama kuna Mbunge yoyote
anaetuhumiwa kwa makosa ya Jinai, Mamlaka za kiuchunguzi zinawajibu wa
kutekeleza majukumu yao na pale inapobidi, Bunge lenyewe kupitia kamati ya
Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge inaweza kufanya uchunguzi kwa Mamlaka ya
Spika.
Aidha, ifahamike vyema kuwa, kwa mujibu wa Kanuni ya
116 (3) Mamlaka ya kufanya mabadiliko kwenye Kamati za Kudumu za Bunge ni ya
Spika na anaweza kufanya hivyo wakati wowote kama alivyofanya mapema mwezi huu
ambapo alizingatia maombi ya baadhi ya Wajumbe 15 kuhamia Kamati nyingine
kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za kiafya kwa baadhi ya Wajumbe na pia
kuboresha Utendaji wa Kamati hizo kama ilivyojitokeza jana kwa wajumbe 27
kuhamishiwa kamati zingine pia. Mhe. Spika anawasihi Wajumbe wote kuendelea
kutekeleza majukumu yao kama kawaida katika kamati zao.
0 comments:
Post a Comment