ZAIDI ya wakazi 400 wa Kijiji cha Iyumbu, Kitongoji
cha Bwibwi katika Manispaa ya Dodoma wamelalamikia Mamlaka ya Ustawishaji Makao
Makuu ya Dodoma (CDA) kupora ardhi waliyokuwa wakiimiliki tangu mwaka 1872.
Wakizungumza na waandishi wa habari kwa wakati tofauti
wakazi hao wamemwomba Rais John Magufuli kuingilia kati mgogoro huo kutokana na
CDA kutaka kuwapokonya ardhi hiyo.
Chifu wa eneo hilo Lazaro Chihoma amesema, eneo hilo
walikuwa wakilitumia tangu miaka hiyo na kwamba, CDA haina haki ya kulitwaa kwa
mabavu.
“Sisi katika eneo hili hatuondoki kabisa, nitupo
tayari hata kufa kwa kuwa hili eneo historia yake ni ya kutoka mwaka 1872
ambapo ndipo babu zetu walianza kuishi hapa.
“Kuna vitu vingi sana vya kihistoria ambavyo kama
CDA watatuondoa hapa, vitakuwa vimekufa kabisa na vizazi vijavyo havitaweza
kuvijua,”amesema Chihoma.
Ameongeza kuwa, watu wamekuwa wakiishi katika eneo
hilo hata kabla ya CDA kuanzishwa miaka ya 70.
Amesema kuwa, CDA wanataka kulimiliki eneo hilo na
kuwaondoa wao ambao ni wakazi halali na kuwapatia watu wengine bila kuwapa
fidia kama vile viwanja hali ambayo inaibua maswali kwao.
Kutokana na hali hiyo, wakazi hao wamemuomba Rais
Magufuli kuingilia kati mgogoro huo ambao una lengo la kuwanyima haki yao ya
msingi.
“Pale CDA kuna majipu mengi na yameiva, tunamuomba
Rais Magufuli aje kutumbua majipu haya bila hivyo CDA itaendelea kuwa kero
kubwa kwa wapiga kura wake,” amesema Chihoma.
Akijibu tuhuma hizo, Paskasi Mlagiri, Kaimu
Mkurugenzi wa CDA amesema kuwa, wakazi hao ni wavamizi.
“Eneo hilo lilikuwa ni msitu, palikuwa hapaishi watu
na sisi tumelichukua toka mwaka 1978 ila kuna mzee mmoja alikuwa analitumia kwa
ajili ya matambiko na palikuwa pori,” amesema Mlagiri.
0 comments:
Post a Comment