MAGARI 213 yanafuatiliwa na Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) baada ya kubainika yameingizwa nchini bila kulipiwa kodi na watu
binafsi pamoja na taasisi mbalimbali zikiwemo za dini. Miongoni mwa magari
hayo, yamo yaliyoingizwa kwa misamaha ya Kituo cha Uwekezaji (TIC) ambayo
(misamaha) imetajwa kutumika isivyo.
Mamlaka imesema inafuatilia kuhakikisha wahusika
sanjari na waliosaidia ukwepaji huo wa kodi, wanachukuliwa hatua. TRA imetaja
majina na taasisi zinazohusika na uingizaji magari hayo, kupitia matangazo kwa
vyombo vya habari na imetoa siku nne wajitokeze kulipia ushuru kabla ya hatua
nyingine kuchukuliwa.
Ukaguzi uliofanywa na mamlaka, ndiyo umebaini kuwepo
kwa magari hayo yaliyoingizwa nchini na kusajiliwa bila kufuata taratibu za
forodha hivyo kuyafanya yamilikiwe bila kulipiwa kodi stahili. Orodha ya magari
213 na namba za usajili, mmiliki na aina ya gari imetolewa katika vyombo vya
habari na mamlaka hiyo imewataka wahusika wajitokeze haraka kulipia gharama
hizo.
Baadhi ya kampuni, taasisi na watu binafsi,
wameingiza magari zaidi ya moja. Miongoni mwa taasisi zilizotajwa kwenye orodha
hiyo zenye magari zaidi ya moja ni JM Hauliers Limited (26), Al-Jabri Co Ltd
(16) na Kampuni ya Dhandho Road Hawlage iliyoingiza 18.
Kampuni nyingine na idadi ya magari yaliyoingizwa
kwenye mabano ni Bamboo Rock Limited (7) na Dayosisi ya Musoma, ambayo hata
hivyo haikufafanuliwa ni ya madhehebu gani ya dini, imeingiza magari manane.
Wengine ni Fai Limited (3), Nam Transport Company (6), Neni Enterprises (2) na
Relief Partner International yenye magari matatu.
Kwa upande wa watu binafsi wenye magari zaidi ya
moja yaliyoingizwa bila kulipia ushuru ni pamoja na Aloyce Kajijira (6),
Mohamed Masoud (5), Mwesige Rwiza (5), Nassor Zakaria (3), Rumishaeli Shoo (3),
Ruwaida Ally (4) Simon Mehi (2), Yahya Hilal (5) na Zahor Issa mwenye magari
matatu.
Wapewa siku nne Akizungumza na mwandishi wa habari
hizi, Mkurugenzi wa Idara ya Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard
Kayombo aliwataka wamiliki wa magari yaliyoorodheshwa kufika katika ofisi
zilizo karibu, wafanyiwe uhakiki walipe ushuru stahiki kabla ya Machi 12 mwaka
huu.
Alisema baada ya tarehe hiyo, TRA itachukua hatua ya
kufuatilia magari hayo na kuyakamata. Alisema ufuatiliaji wa magari
yaliyoingizwa nchini bila kulipiwa ushuru ni endelevu. Waliouziwa matatani
Akizungumzia watakaokuwa wameuziwa magari hayo bila kufahamu kama yalitolewa
bila kulipiwa kodi stahili, Kayombo alisema pia wanatakiwa kujitokeza.
Alisema walioyanunua magari hayo, ambayo namba zake
zimeoneshwa, wanapaswa kujitokeza wapigiwe hesabu, walipe kiasi kinachodaiwa na
mamlaka. Kwa mujibu wa Kayombo, watakapofika katika ofisi za TRA, zitafanyika
taratibu kuangali jinsi ya kulipa, kwani yapo magari ambayo hayakulipiwa kabisa
au yamelipiwa kidogo kutokana na kufanya udanganyifu katika malipo. Waliosaidia
ukwepaji kodi Hata hivyo, Kayombo alisema baada ya kulipa gharama hizo, hatua
nyingine zitachukuliwa.
Hatua hizo za kisheria, zitahusu waliopitisha magari
hayo na waliosaidia katika kufanya udanganyifu wa kulipa kodi stahiki kwa
magari hayo. Jipu lingine Kubainika kwa magari hayo ni mwendelezo wa TRA,
kudhibiti ukwepaji kodi baada ya hivi karibuni, kubaini waliokwepa kodi kwa
kupitisha kontena kwa njia ya udanganyifu.
Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk Philip Mpango hivi
karibuni alikaririwa akisema serikali haitafumbia macho watu watakaobainika
kutumia TRA kama pango la kujinufaisha kiuchumi. Dk Mpango alieleza kukerwa na
vitendo vya ubadhirifu vinavyofanywa na baadhi ya watumishi wa mamlaka hiyo ya
kodi wasio waaminifu.
Taarifa za hivi karibuni zinaonesha, TRA katika
kukabiliana na wakwepa kodi, imekusanya Sh bilioni 11.8 kutoka kwa wafanyabiashara
waliokuwa wameondosha makasha yao katika Bandari Kavu kinyume na taratibu za
forodha.
Kaimu Kamishna wa TRA, Alphayo Kidata alisema hivi
karibuni kwamba, makusanyo hayo yanajumuisha Sh bilioni 5.3 ambazo zimetolewa
na kampuni na wafanyabiashara 19, ambao awali hawakulipa kodi za kontena zao na
wengine 19 ambao wamelipia sehemu ya kodi ya kontena zao.


0 comments:
Post a Comment