BAADA ya Rais John Magufuli kusitisha uingizaji wa
sukari kutoka nje ya nchi ili kulinda na kufufua viwanda vya ndani, kumekuwa na
malalamiko katika siku za hivi karibuni kwamba bidhaa hiyo imepanda bei ghafla.
Kabla ya agizo hilo, sukari ilikuwa inauzwa kati ya
Sh 1,800 hadi Sh 2,200 lakini taarifa ambazo zimekuwa zikitolewa na wananchi
zinaonesha kwamba bei ya sukari katika baadhi ya maeneo imepanda hadi kufikia
Sh 2,600.
Dhana iliyokuwepo kutokana na kupanda kwa bei ya
sukari ghafla baada ya zuio la Rais ilikuwa kwamba huenda viwanda vyetu bado
havikidhi mahitaji ya soko la ndani. Lakini tunashukuru taarifa ya Bodi ya
Sukari kuonesha kwamba upatikanaji wa sukari nchini ni wa kuridhisha na ipo
akiba ya kutosheleza nchi nzima.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania, Henry
Simwanza, amekaririwa na gazeti hili akisema kwamba pamoja na baadhi ya viwanda
kusimamisha uzalishaji wa sukari kutokana na msimu kuisha, hali ya sukari
nchini ni nzuri kwani ipo akiba zaidi ya tani 62,000.
Mkurugenzi huyo anasema bodi yao imegundua kwamba
kuna wafanyabiashara wakubwa ambao kwa sababu wanazozijua wenyewe wameamua
kuficha sukari ili kusababisha upungufu na hivyo kupandisha bei.
Sisi tunadhani huenda pia wanafanya hivyo ili
kuikomoa serikali na hatimaye iwaruhusu kuendelea kuingiza tena sukari kutoka
nje inayowapa faida maradufu. Bodi ya Sukari imeweka wazi kwamba wanaofanya
hujuma hizo watakapobainika watachukuliwa hatua za kisheria.
Imewataka wafanyabiashara kuuza sukari kwa bei
elekezi ambayo ni Sh 1,800 kwa kilo katika jiji la Dar es Salaam na mikoa ya
jirani. Sukari ni moja ya bidhaa muhimu kwa familia nyingi kwa sababu inatumika
katika kutayarishia vyakula vingi.
Yapo mazingira ambayo hali ikiwa mbaya kimapato,
familia inaweza kupitisha siku kwa kunywa uji, na ili hilo lifanikiwe ni lazima
iwepo sukari. Kama hata bei ya bidhaa hiyo familia haitamudu hali inakuwa mbaya
zaidi.
Sukari pia ninawezesha akina mama kufanya biashara
za maandazi na vitumbua na hivyo kujiongezea kipato. Sukari inapopanda bei
inakwamisha pia biashara hizo kutokana na kipato kidogo cha wananchi walio
wengi.
Ni kwa msingi huo, tunaunga mkono kwa dhati juhudi
za Bodi katika kupambana na watu wanaosababisha bidhaa hii muhimu kupanda bei.
Tunaiomba Bodi isiishie katika kutoa onyo pekee, bali kuanza uchunguzi wa kina
na kuchukua hatua stahili kwa kila atakayebainika kuhujumu agizo la Rais.
Kama alivyosema Mkurugenzi wa Bodi, Simwanza, ni
vyema kila mwananchi asaidie kuwafichua watu wanaoficha sukari ili kupandisha
bei na kufifisha juhudi za serikali za kufufua viwanda vya sukari, hatua ambayo
pia ni faida kwa wakulima.
Tunaamini kwamba juhudi hizi zikiungwa mkono
ipasavyo, tunaweza kuzalisha sukari ya kutosha na hata kuuza nje ya nchi, hatua
itakayokwenda sambamba na kupanua maradufu kilimo cha miwa nchini.


0 comments:
Post a Comment