Kiungo wa Azam FC, Farid Mussa (kulia) akimtoka beki
wa Esperance, Yacine Rabii(Picha Na BinZuberi).
Na Somoe Ng'itu, DAR ES SALAAM
AZAM FC imejiweka kwenye nafasi ya kwenda hatua ya
mchujo wa kuwania kupangwa kwenye makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Hiyo inafuatia ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya
Esperance ya Tunisia jioni ya leo katika mchezo wa kwanza wa hatua ya 16 Bora
Kombe la Shirikisho Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Shukrani kwao, wachezaji vijana wadogo Farid Mussa
Malik na Ramadhani Yahya Singano ‘Messi’ waliofunga mabao hayo kipindi cha pili
baada ya Azam FC kuwa nyuma kwa 1-0 tangu kipindi cha kwanza.
Azam FC inayomilikiwa na Alhaj Sheikh Said Salim
Awadh Bakhresa na familia yake sasa inatakiwa kwenda kulazimisha sare yoyote
ugenini katika mchezo wa marudiano wiki ijayo ili kwenda hatua ya mwisho ya kuwania
kucheza hatua ya makundi.
Esperanace walipata bao lao dakika ya 33 kupitia kwa
Haithem Jouini aliyefunga kwa kichwa akimalizia krosi ya Ilheb Mbaark.
Nahodha John Bocco alipoteza nafasi zaidi ya mbili
za wazi kipindi cha kwanza, ikiwemo dakika ya 22 baada ya kupiga nje akiwa
amebaki yeye na kipa.
Mshambuliaji mwingine tegemeo wa Azam, Kipre Herman
Tchetche alipoteza nafasi nzuri dakika ya 36 baada ya kupiga juu akiwa mbele ya
lango.
Kipindi cha pili, mabadiliko yaliyofanywa na kocha
Muingereza Stewart Hall kumtoa kiungo Muivory Coast, Kipre Michael Balou na
kumuingiza mzawa, Frank Raymond Domayo yalirejesha uhai kwenye kikosi cha Azam.
Na hapo ndipo Azam FC walipofanikiwa kubadilisha na
matokeo ya mchezo pia kutoka kuwa nyuma kwa 1-0 hadi kuongoza kwa 2-1.
Farid alianza kufunga dakika ya 68 baada ya
kutanguliziwa pasi fupi na Singano Messi.
Kiungo wa zamani wa Simba, SIngano ‘Messi’
akaifungia bao la ushindi Azam dakika ya 70, safari hiyo naye akisetiwa na
Farid Mussa kwa krosi nzuri kutoka upande wa kushoto.
Esperance walionekana kupagawa na mabao hayo mawili
ya haraka na kuwaruhusu Azam kuongeza mashambulizi langoni mwao.
Beki Muivory Coast, Serge Wawa alishindwa kuendelea
na mchezo dakika ya 89 baada ya kuumia misuli na nafasi yake kuchukuliwa na
David Mwantika aliyemalizia mchezo vizuri.
Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Aishi Manula, Erasto
Nyoni, Waziri Salum/Khamis Mcha ‘Vialli’ dk67, Aggrey Morris, Serge Wawa/David
Mwantika Serge Wawa dk89, Jean Baptiste Mugiraneza, Kipre Tchetche, Kipre
Bolou/Frank Domayo dk46, Ramadhani Singano ‘Messi’, John Bocco na Farid Mussa.
Esperance: Moez Ben Cherifia, Iheb Mbaarki, Yacine
Rabii, Mohamed Ali Yaakoubi, Chamseddine Dhaouadi, Hoiucine Regued, Fousseny
Coulibaly, Driss Mhirsi, Ilyes Jelassi/Adem Rjaibi dk75, Fakhreddine Ben
Youssef na Haithem Jouini.
0 comments:
Post a Comment