AZAM FC wameanza mikakati kabambe ya kuwamaliza
wapinzani wao timu ya Esperance ya Tunisia katika hatua ya 16 bora ya Kombe la
Shirikisho, baada ya kuifanyia ‘ushushushu’ kwa kuwasoma ‘live’ katika mchezo
wao wa Ligi Kuu uliochezwa juzi nchini humo.
Esperance wanaoshika nafasi ya tatu katika msimamo
wa ligi, walitoa kipigo cha bao 2-1 dhidi ya vibonde Club African wanaoshika
nafasi ya 11, mchezo ambao ulishuhudiwa na kocha msaidizi Denis Kitambi na
Ofisa Mtendaji Mkuu, Saad Kawemba.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Kawemba alisema wapo
jijini Tunis kuwasoma wapinzani wao, pia kuandaa mazingira watakapofikia
wachezaji pindi timu itakapowasili nchini humo kwa mchezo wa marudiano.
“Tulichokuwa tunataka ni kuangalia namna gani
wanacheza wakiwa katika mchezo wa ushindani kama tulivyowaona kwenye mechi ya
ligi jana (juzi), hata hivyo tutaendelea kuwatazama kupitia kwenye video tulizonazo ili kuendelea kuwasoma
kimbinu.
“Katika mchezo wao huo dhidi ya Club African,
tulishuhudia wachezaji wawili wa timu hiyo wakipewa kadi nyekundu, hali
inayotupa tahadhari kwamba tukicheza nao kuwe na nidhamu ya kimchezo,” alisema
Kawemba.
Akieleza nini wamejifunza kutokana na mchezo huo,
Kawemba alisema uzito wa mechi ya Tunisia, utategemea zaidi matokeo ya mchezo
wa kwanza utakaochezwa Dar es Salaam Jumapili hii.
“Kwa ufupi kwa matokeo yoyote Dar es Salaam mechi
bado haitakua imekwisha, matokeo ya michezo miwili ni muhimu sana,” alisema.
0 comments:
Post a Comment