WANACHAMA wa Chama cha Wananchi (CUF), wameanza
kushikana uchawi, huku viongozi wakitakiwa kutoa maelezo ya kwanini wameshindwa
kujadili hatua ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa
Ibrahim Lipumba.
Pamoja na hali hiyo,wanachama hao wamemtaka Katibu
Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad kutambua kuwa ana wajibu wa
kuwasiliana na Profesa Lipumba ili arejee katika nafasi yake ya zamani kwa
mujibu wa katiba ya chama hicho.
Hayo yamesemwa Dar es Salaam wakati wa kongamano lililoandaliwa na Kata ya Makurumla
Manispaa ya Kinondoni, ambapo mmoja wa wana CUF Mohamed Mgomvi, alisema
anashangazwa na hatua ya kikao cha Baraza Kuu kushindwa kujadili barua ya kujiuzulu
Profesa Lipumba.
Alisema CUF kwa upande wa Bara, imebaki haina mtu
madhubuti ambaye anaweza kukiendesha kama alivyokuwa kiongozi huyo.
“Ninashangaa hapa mzee Wandwi (Mustafa), kama
Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa chama unashindwa kusema ukweli. Leo hii
(jana) CUF imebaki yatima tangu alipoondoka Profesa Lipumba halafu mnasema tupo
naye pamoja.
“Haiingii akilini hata kidogo, ni unafiki umetawala
kwa baadhi ya viongozi ambao kila kukicha wanakutana na Lipumba wanamuonyesha
wanamhitaji, akitoka mnamsema vibaya.
“…napenda kukuambia leo CUF hakuna mwenye uwezo wa
kuvaa viatu vya Profesa Lipumba tunamhitaji kiongozi wetu, tumechoka kuburuzwa
na unafiki unaoendelea ndani ya chama,” alisema Mgomvi.
Naye Mangaa Dachi, alisema kwa mujibu wa katiba ya CUF barua ya
kujiuzulu Profesa Lipumba inatakiwa iwasilishwe katika kikao cha mkutano mkuu uliomchagua
kuliko ilivyo sasa.
“Hivi mnajua kama chama tunavunja Katiba? Kama
ndivyo hivyo bado suala la Profesa Lipumba linatakiwa kuwasilishwa kwenye
mkutano mkuu, nasi tunamtaka Lipumba arudi katika nafasi yake,” alisema Dachi.
Pamoja na hali hiyo wanachama hao walilalamikia
mfumo wa upatikaji wa wabunge wa viti maalumu ndani ya chama hicho kuwa umekuwa
ukihusishwa na tuhuma za rushwa kwa baadhi ya wakurugenzi.
“Hatuwezi kuvumilia hali hii hata mfumo wa upatikaji
wa wabunge wa viti maalumu hivi sasa watu wanafanya wanavyojisikia, leo
kuondoka kwa Lipumba wapo baadhi ya wakurugenzi wanatajwa kuchukua fedha kutoka
kwa baadhi ya wabunge waliopo sasa ili wawape ubunge,” alisema.
Akifungua kongamano hilo, Mkurugenzi wa Ulinzi na
Usalama wa CUF, Mustafa Wandwi, alisema pamoja na yanayoendelea bado wako
pamoja na Profesa Lipumba kwa kila jambo linaloendelea ndani ya chama hicho.
Alisema kutokana na hoja ya washiriki wa kongamano
hilo, bado kuna kila sababu ya kutafakari kwa kina suala la Profesa Lipumba
lakini hata katika kikao cha Baraza Kuu la Uongozi kilichofanyika hivi karibuni
visiwani Zanzibar, suala hilo lilijadili kwa kina.


0 comments:
Post a Comment