Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano inapenda
kutaarifu Umma kuwa Daraja la kigamboni litaanza kutumika siku ya Jumamosi
tarehe 16, Aprili, 2016 kuanzia saa 12:00 asubuhi.
Katika siku za mwanzo, magari yatapita bila kulipia
tozo hadi Serikali itakapokamilisha taratibu na kutangaza utaratibu wa
kulipia. Aidha, watembea kwa miguu na
waendesha baiskeli watavuka bure katika Daraja la Kigamboni.
Hata hivyo maguta na mikokoteni haitaruhusiwa
kutumia daraja hilo kutokana na sababu za kiusalama.
Magari yatakayoruhusiwa kupita katika Daraja la
Kigamboni katika siku hizo za mwanzo ni yale yenye uzito usiozidi tani 10,
hatua ambayo itasaidia kufuatilia mwenendo wa upitaji wa magari katika daraja,
barabara za juu (Interchange) katika eneo la Kurasini, pamoja na kuhakikisha kwamba
magari yanayotoka au kuingia katika daraja hayasababishi msongamano wa magari
katika Barabara ya Nelson Mandela, Barabara ya Kilwa na maeneo mengine ya
jiji. Baada ya utaratibu kukamilika
magari ya aina zote yenye uzito unaoruhusiwa kisheria yataruhusiwa kupita
katika daraja.
Mambo muhimu ambayo madereva na watumiaji wengine wa
barabara wanatakiwa kuzingatia ni:-
1) Kuzingatia sheria ya Usalama Barabarani ikiwa ni
pamoja na kufuata mwendo kasi unaotakiwa ili kuepuka ajali na kuepuka uharibifu
miundombinu ya daraja
2) Kufuata alama za barabarani zilizowekwa katika
‘Interchange’ ya Kurasini ili kwenda kwenye uelekeo sahihi.
3) Kuzingatia alama zilizowekwa kwenye milango (Toll
Gates) ya Kituo cha kulipia tozo (Toll Plaza) ili kuepuka uharibifu wa miundombinu
ya kituo hicho.
4) Madereva na watumiaji wa barabara wengine
watakaosababisha uharibifu wa aina yeyote wa miundombinu ya daraja watatozwa
faini au kuchukuliwa hatua nyingine za kisheria.
5) Kutunza mazingira kwa kuepuka kutupa takataka
katika eneo la daraja.
Aidha, Wizaraya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
inawataka madereva wa magari ya mizigo wanaoegesha katika barabara ya Nelson
Mandela wakisubiri kuingia bandarini watafute eneo stahiki la maegesho na
kuyaondoa magari hayo kwani hatua za kisheria zitachukuliwa kwa wale watakaoenda
kinyume na agizo hili.
Msongamano wa magari hayo husababisha uharibifu wa
barabara na usumbufu mkubwa kwa watumiaji wa barabara katika eneo hilo.


0 comments:
Post a Comment