Katika kujadili hali hiyo, TEF imeguswa kwa namna ya
kipekee kabisa na mwenendo mzima wa urushaji wa bahari za Bunge kwa njia ya
redio na luninga, hususan katika mkutano wa tatu wa Bunge la 11 unaoendelea
mjini Dodoma kwa sasa.
Itakumbukwa kwamba Muhimili wa Bunge kupitia Kitengo
chake cha Habari, Elimu na Mawasiliano, Aprili 15 2016 ulitoa taarifa kwa umma
ikieleza utaratibu mpya ambao sasa umeanza kutumika katika kurusha matangazo ya
redio na luninga kutoka Bungeni.
Katika taarifa hiyo, Ofisi ya Bunge ilisema kuwa
imeamua kuboresha mfumo wa urushaji wa Matangazo ya Bunge kwa Bunge lenyewe
kurusha Matangazo ya Vikao vyake pamoja na Vipindi mbalimbali vyenye Maudhui
kuhusu Shughuli za Bunge ambazo hazijapata fursa ya kufahamika vyema kwa umma
kuanzia katika Mkutano wa Bunge la Bajeti unaoendelea sasa.
Ofisi hiyo ilisema kuwa mfumo huo mpya ni Utamaduni
wa kawaida kwa kila Bunge hususani Mabunge ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya
Madola kuwa na Studio zake kwa lengo la kurusha Matangazo ili yawafikie wadau
kwa lengo la kurusha kupitia vituo vyao.
Kwa maana hiyo, Bunge lilisisitiza kuwa chini ya
utaratibu huo mpya, jukumu la kurusha Matangzo ya Vikao vya Bunge litafanywa na
Bunge lenyewe kupitia FEED MAALUM ili kurahisisha kila Kituo cha Radio na
Televisheni kupata Matangazo hayo kwa sehemu walipo bila kufunga Mitambo yao
Bungeni Dodoma.
Katika kutekeleza uamuzi huo na mfumo huo mpya, kila
kituo cha Televisheni na Redio sasa watatumia Masafa ya Matangazo ya Bunge
(Frequencies) bure kupitia FEED MAALUM itakayorushwa na Satellite ya INTELSAT
17 ambayo iko nyuzi 66 Mashariki kwa masafa maalum ambayo pia yaliwekwa wazi.
Kwa mantiki hiyo, Bunge sasa limezuia vituo vyote
vya televisheni nchini kupeleka kamera zake ndani ya Bunge kwa kuwa habari hizo
zitapatikana kwenye feed maalum ambayo ni ya Bunge ambayo inasimamiwa na
waandishi wa Bunge ambao pia ndio wanaamua nini kionyeshwe kwa utashi wao.
Baada ya kutafakari hatua hizi mpya za Bunge na baada
ya kufuatilia kile kinachorushwa, mambo kadhaa yamethibitika:-
Mosi, habari kutoka ndani ya Bunge sasa zinachujwa
mno kupitia mfumo huu mpya wa feed maalum;
Pili, ubora za picha zinazorushwa kupitia feed hii nao
ni wa kiwango cha chini pia;
Tatu, kwa mantiki ya kawaida kabisa, hatua hizi zote
zimepunguza na kukwaza haki ya wanahabari kufanya kazi yao kwa uhuru, lakini
pia inawanyima wananchi haki ya kupata kwa uhakika na bila kuchujwa kile kinachofanywa
na wawakilishi wao.
Kwa kuzingatia haya yote, TEF inasema bayana kwamba:
Hatua hizi
mpya za kuzuia kamera za televisheni kuingia Bungeni ni hatua za dhahiri kabisa
za kukwaza uhuru wa habari nchini na kukuza censorship nchini. Hali hii
haisaidii siyo Bunge tu, bali hata wabunge, wananchi na taifa kwa ujumla katika
kupiga hatua za kweli katika kujenga demokrasia na kulinda haki za kupata
habari na uhuru wa kujieleza nchini;
TEF
imeanza kuingiwa na hofu kwamba sababu za awali zilizokuwa zimetolewa za kuzuia
utangazaji wa moja kwa moja wa Bunge kupitia TBC kwa sababu ya gharama, huenda
hazikuwa za dhati. Hali hii imejionyesha hasa baada ya vituo binafsi vya
televisheni kujitokeza na kuendelea kuonyesha vikao vya bunge moja moja, lakini
navyo sasa vimenyimwa fursa hiyo kwa utaratibu huu mpya wa feed maalum.
Ni dhahiri
sasa, ushiriki wa wananchi katika kufuatilia mwenendo wa Bunge na wabunge wao
umekwazwa sana kwa hatua hizi mpya na kwa maana hiyo, kupunguza ushiriki wa
wananchi katika mfumo wa utawala wa nchi yao.
Kwa kuzingatia haya yote, TEF inatoa rai kwa uongozi
wa Bunge kufikiria upya hatua hizi za kuzidi kufunika shughuli za Bunge kwenye
blanketi zito la usiri na censorship, hivyo uruhusu kituo chochote cha
televisheni chenye nia, uwezo na utayari wa kurusha matangazo ya Bunge moja
moja bila kulazimika kujiunga na feed maalum iliyoanzishwa.
Tunaamini kwamba kama hali hii ya kutumia feed
maalum itaachwa iendelee hakika Tanzania kama taifa tunapiga hatua nyuma kwa
yale mazuri machache tuliyokuwa tumeyafikia, mojawapo, uhuru wa Bunge kuendesha
mambo yake kwa uhuru na uwazi mkubwa hivyo kuwa mfano mojawapo wa taasisi za umma
zinazojiendesha kwa uwazi.
Imetolewa leo, Jumapili Aprili 24 2016 jijijni Dar
es Salaam na Jukwaa la Wahariri Tanzania.
Theophil Makunga Neville Meena
Mwenyekiti Katibu
0 comments:
Post a Comment