LICHA ya miundombinu ya barabara kuboreshwa usafiri
wa reli bado unapaswa kuwapo kutokana na umuhimu wake hasa katika kurahisisha
usafirishaji.
Mizigo mingi inayosafirishwa na malori, iwe ndani
ama nje ya nchi, inaweza kusafirishwa kwa njia ya reli na kuondoa msongamano wa
malori pamoja na makontena bandarini kama ilivyo sasa.
Usafiri wa gari moshi bado una umuhimu katika
usafirishaji kwani gari moja linaweza kubeba hadi makontena 50 yenye urefu wa
futi 40 kwa mara moja, hivyo kurahisisha usafirishaji na kupunguza gharama za
uchukuzi wa mzigo huyo.
Rais Dk. John Magufuli aliahidi kuimarisha mtandao
wa reli kama alivyofanya kwenye barabara wakati akiwa waziri wa ujenzi.
Ikiwa ni pamoja na kuwashawishi wazalishaji wa
viwanda nchini kutumia njia za reli kusafirishia shehena ya bidhaa zao kwenda
ndani na hata nje ili kudhibiti uharibifu wa barabara lakini kupunguza gharama
za usafirishaji.
Ahadi hiyo imeanza kutekelezwa baada ya hivi
karibuni Kampuni ya Saruji Tanga kusaini mkataba wa makubaliano na Shirika la
Reli Tanzania (TRL) kusafirisha tani 35,000 za saruji kwa njia ya reli.
Makubaliano hayo ambayo yalishuhudiwa na Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, yalifanyika katika
kiwanda hicho kilichopo Tanga.
Makubaliano hayo yataongeza safari za TRL katika
njia ya Tanga na kuipatia kampuni hiyo suluhisho la usafirishaji wa shehena ya
bidhaa ya saruji inayozalishwa na kiwanda hicho kwa gharama nafuu.
Waziri Mbarawa anasema kupitia makubali hayo TRL
imeandika historia mpya kwa kuanza tena kusafirisha shehena kubwa ya mzigo kama
hapo zamani.
Anasema kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitano toka
kurejea tena shirika hilo limekuwa likisafirisha shehena ya mizigo tani 150,000
hadi 200,000 kwa mwaka pekee.
“Hivyo kwa usafirishaji wa tani 35,000 kwa mwezi ina
maana kwa mwaka mzima TRL itakuwa na uwezo wa kusafirisha saruji tani 420,000
mzigo ambao ni mkubwa kuwahi kusafirishwa na shirika hilo kwa kipindi kirefu,”
anasema Profesa Mbarawa.
Anasema kupitia usarifishaji huo shirika
linatarajiwa kutengeneza faida ya Sh milioni 40 kwa kusafirisha shehena ya
mzigo kwa mwezi kutoka Tanga – Kigoma – Mwanza.
“Lengo la serikali ni kuwezesha viwanda vyetu
kuzalisha kwa wingi lakini pia kuweka miundombinu bora ambayo itawezesha bidhaa
kumfikia mlaji kwa haraka na kwa gharama nafuu ili kuwakomboa wananchi wetu
kiuchumi,” anasema.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TRL, Masanja Kadogosa,
anasema makubaliano hayo yatawezesha shirika lake kusafirisha shehena ya saruji
inayozalishwa kiwandani hapo kwa urahisi na kuisambaza maeneo mbalimbali.
Anasema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji ambao
walishauanza mwaka 2014/15 ambapo kiwanda cha saruji kiliweza kusafirisha tani
44,000 kupitia njia ya reli.
Hivyo kufuatia ongezeko la shehema hiyo shirika lake
limeweza kutenga vichwa vitano vya treni na kimoja cha shanta maalumu kuhudumia
kampuni hiyo ya saruji.
“Tunatarajia kusafirisha shehena ya saruji zaidi ya
tani 20,000 kwa mwezi kutoka kiwandani hapo hadi Kigoma na tani 15,000 kutoka
Pongwe kuelekea Mwanza,” anasema Kadogosa.
Anasema kiwanda hicho kitakuwa kimepata suluhisho
madhubuti la usafirishaji wa mizigo mikubwa na mizito jambo litakalowanufaisha
wateja wa kampuni hiyo na Watanzania
Mkurugenzi huyo ameiomba kampuni hiyo kulipa gharama
za usafirishaji kwa wakati ili kusaidia shirika hilo kutoa huduma bora.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo,
Reinhardt Swart, anasema mkataba huo utawezesha kusafirisha saruji tani 35,000
ujazo ambao ni theluthi ya tani 105,000 inayozalishwa kiwandani hapo kwa mwezi.
Anasema kampuni yake itaongeza ufanisi katika
uzalishaji ili kuleta ushindani katika soko pamoja na kupunguza gharama za
usafirishaji.
“Kumekuwapo na malalamiko kwa wateja wetu kuhusu
gharama za saruji lakini tulikuwa tunatumia gharama kubwa katika usafiri kwa
njia ya barabara, ambapo wakati mwingine bidhaa ilikuwa inachelewa kufika kwa
wakati kutokana na changamoto zilizopo barabarani,” anasema Swart.
Swart anasema matumizi ya reli yanazingatiwa duniani
kote kama njia stahiki ya usafirishaji yenye gharama nafuu na athari ndogo za
kimazingira ukilinganisha na usafiri wa barabara.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigella, anasema
mkoa utaendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji ili wawekezaji hao waendelee
kuwekeza na kuongeza pato la uchumi la mkoa.


0 comments:
Post a Comment